KURUNZI
YA KANISA FM
Wakati umenipa kibali
ili niweze kukuletea habari jamali. Asanti sana kwa kujiunga nami nikikumulikia
yaliyojiri kwa ijili. Lakini kwanza kawaida yetu ni kuvipata vimulimuli.
VIMULIMULI
- Kinyesi kikavu chapika...
- Tutaangalia vita
dhidi ya wanamgambo wa kiroho...
- na Michezoni Nehemia
ashinda Tobia.
Hujambo na karibu mimi
ni msimulizi wako Paul King’ori.
KURUNZI
TIMILIFU
TAHADHARI:
Mwelekezi wangu ananiarifu kuwa habari ifuatayo yaweza kuzua hisia
zisizoridhisha hususan kama watafuna. Hata hivyo, ni ukweli mtupu... Nabii
Ezekieli alipitia mateso ya aina yake huko Yerusalemu. Licha ya kuagizwa alalie
kaure kwa siku 390, alikuwa anafungwa kwa kamba na Mungu ili asipinduke. Hii ni
ishara ya vile Israeli watakavyofungwa utumwani. Hicho kilikuwa ni kionjo cha
kiroja. Kilele chake kilikuwa cha kushangaza zaidi. Uhalisia ni kuwa kinyesi
hutumika kuzalisha kawi. Aghalabu kawi yenyewe hutumika kupikia. Hata hivyo,
mwenyezi Mungu alimweleza Ezekieli apike
kwa kinyesi cha binadamu. Ndiyo, cha binadamu. Mungu alimwamuru nabii huyo aoke
mkate kutumia kinyesi kikavu. Haya yanaashiria uchafu wa dhambi za Yerusalemu.
Ezekieli alipewa maelezo hayo na alipomlalamikia Mungu ya kuwa hajajichafua,
Mungu alimhurumia na akamwambia aoke mkate wake kwa kinyesi cha ng’ombe kama
mbadala. Hii ikawa ni ishara ya vile watakavyokula chakula kichafu kwa kuzidiwa
na dhambi.
Hayakuishia hapo. Aliambiwa anyoe ndevu na
kichwa chake, kisha aigawe nywele aliyokata katika matuta. Alikuwa achome
thuluthi moja, thuluthi nyingine aikate kwa upanga na nyingine aitawanye kwa
upepo. Ya Mungu ni mengi na hiyo ni gharama ya dhambi dhidi yake. Ripoti hii ni
kutoka Ezekieli 4 na 5.
Nyakati hizi za kisasa,
nchi nyingi zimeshuhudia uhaba wa chakula. Hata hivyo gatuzi la Galilaya
lilipata chakula cha msaada kutoka mbinguni (ama ukipenda Heaven For Galilee).
Haya yalifuatia baada ya siku tatu za makali ya njaa. Makamu wa Rais aliwaonea
huruma na kufanyia mikate mitano na samaki wawili mujiza. Bidhaa hizo zilikuwa
chakula kingi mno cha thamani ya mamilioni ya pesa. Chakula hicho kiliishibisha
halaikiya watu elfu tano! Kwa mujibu wa mmoja wa waliokula, aliyejitambulisha
kama Mariko, alisema kilikuwa kitamu kupindukia na hata walibakisha vikapu kumi
na viwili.
Kinaya ni kuwa mujiza huu haukulipishwa kama
miujiza mingi ya siku hizi. Kwa habari zaidi, tumia anwani ya mtandao ifuatayo.
Holybible@ mark6.36-41.com
KURUNZI
BIASHARA
Huku shilingi ya Kenya ikiendelea kupoteza
thamani kwa kasi, nchi ya Yerusaremu hivi karibuni huenda ikaanza kulia
kivulini. Walakini lazima wananchi wafuate masharti ya Mwenyezi Mungu.
Inawalazimu kutupilia mbali dhambi zao. Kulingana na kituo cha habari cha Isaya
55.1, Wanayerusaremu wataanza kula mikate na kunywa divai na maziwa bila kulipa
hata thumni! Haya yatawezeshwa na Mungu mwenyewe ili wajue kuwa yeye ndiye
Mungu Muumba na kwamba yuamiliki kila
kitu duniani. Wito wa usaidizi huo umepeanwa na Mola kupitia kwa msemaji wake
nabii Isaya, huku akisema kuwa nia zenu si kama zake wala mawazo yake kama yenu.
KURUNZI
KIMATAIFA
Hivi karibuni tumeshuhudia vita baina ya
jeshi la Kenya na wanamgambo wa Al-Shabaab. Aghalabu vita hufanyika baina ya
watu au nchi. Hii ni dhihirisho tosha kuwa vita ni vya aina nyingi. Uhalisia ni
kuwa sisi Wakristo hatupigani vita vya kimwili ila twapigana vya Kiroho dhidi
ya mwovu na ujanja wake. Hivyo basi ni muhimu kutumia silaha za kiroho, ili
tushinde hivi vita. Baadhi ya silaha hizi ni; Mshipi wa Ukweli, kifuani tuvalie Utakatifu,
viatu vya Ubashirina, ngao ya Imani, helmeti ya Wokovu na sime ya Neno la
Mungu. Aidha tutumie gari la Maombi.
Usaidizi wa Mungu utakaotokana na maombi ndio utakaokuwa mafuta ya magari yenu.
Hii ni ripoti kutoka waraka wa Paulo kwa Waefeso 6:10-18.
KURUNZI
MICHEZONI
Katika michezo, timu ya Nehemia iliihemesha
timu ya Tobia na Sanbalati huko Yerusalemu. Timu ya Sanbalati ilikuwa imekula
njama ya kumchezea Nehemia vibaya,
kumjeruhi uwanjani na hatimaye kumuua. Ilifumbuliwa kuwa Sanbalati
walikuwa wamepanga kumtega Nehemia uwanjani wa kujengea Ukuta. Hata hivyo
Nehemia aliikwepa mikiki ya Tobia na kukataa kula mtama aliomwagiwa na
akaendelea na kazi ya ujenzi wa ukuta. Hapo ndipo alipowafungia mabao saba kwa
nunge kwani hawakumpata wamdhuru. Ripoti hiyo ya Nehemia 6 ndiyo inatukamilishia
Kurunzi kwa sasa. Asanti kwa kunipa makini yako. Mungu akubariki na ukumbuke
kumwombea mwenzako. Hadi wakati mwingine, mimi ni Paul King’ori.
No comments:
Post a Comment