Monday 17 September 2012

KURUNZI YA KANISA FM 7



  15.09.2012
KURUNZI YA KANISA FM
“Njooni sasa, tutafakari pamoja.” Asema Bwana. Hayo ni maneno yake nabii Isaya. Yanatoka Isaya 1:18, na ndiyo maudhui ya Wikendi hii ya Washiriki. Ni wito wake Mungu ili tutoke dhambini na tumrejelee. Mengi tunayo kutoka gatuzi la Uasin Gishu na nje ya nchi, lakini kwanza tuvipate vimulimuli.
Ø Tutamulika Misheni ya Chuoni mwaka wa 2013...
Ø Tutakueleza kuhusu suti ya Wesonga...
Ø ... Na Michezoni tutamulika Uogeleaji.
Moja kwa moja kutoka Jumba la Inspiration House, barabara ya Biblical Avenue, hii ni Kurunzi Ya Kanisa FM. Karibu tukutaarifu kitimilifu, mimi ni King’ori Wangechi.
KURUNZI TIMILIFU
Hii ni wikendi ya kipekee ambayo tunajiunga na washiriki. Hawa ni waliokamilisha masomo yao, na huduma mbalimbali miaka iliyopita hapa chuoni na kanisani mtawalia. Ni wikendi iliyojaa shughuli tele zinazowahusisha washirika na washiriki. Furaha nyingi imeonekana nyusoni mwa wote. Hata hivyo, wikendi hii ya washiriki inaletwa kwenu kwa hisani ya Misheni ya Chuoni (Varsity Mission 2013).
Misheni ya Chuoni ni mpango unaotekelezwa kila baada ya miaka mitatu. Misheni hii ni ya kuwahubiria wote walio ndani na nje ya chuo. Ni mpango utakaofanyika mapema mwakani. Misheni yenyewe itajumuisha shughuli kama mikutano ya kufufua, siku ya mazingira, siku ya kunadhifishwa kwa kila mtu bila malipo, semina na nyimbo za sifa na pambio. Wahubiri na waimbaji wanaotambulika kitaifa na kimataifa wataalikwa, kushiriki. Nyote mwaalikwa ili tuanze kuhubiri Yerusalemu yetu iliyo chuo kikuu cha Moi. Hapo tutakuwa tumetimiza matakwa yake mwokozi kama yalivyo katika Luka 24:47,
“Na kwamba mataifa yote watahubiriwa kwa jina lake habari ya toba na ondoleo la dhambi kuanza tangu Yerusalemu.”
Misheni ya mwaka ujao ni tofauti na ingine yoyote. Hii imeandaa matembezi ya Amani huko Langas mjini Eldoret.
Matembezi hayo yatafanyika tarehe 29 Septemba mwaka huu. Yatafanyika vijijini vya Kisumu Ndogo, Yamumbi, Kasarani na Kahuruko. Hizi ni sehemu ambazo ziliathiriwa zaidi na ghasia za baada ya uchaguzi uliopita. Kamati andalizi ya Misheni ya chuoni ikaona ni hekima kuwa na matembezi ya Amani.
 Pauline Kachinja, mwenyekiti wa kamati andalizi ya matembezi ya Amani alinukuliwa na kanisa FM akisema kuwa sio matembezi ya siku moja tu, halafu mambo yawe basi, bali ni mpango unaonuiwa kuendelea na lengo lake ni kudumisha amani kati ya kabila tofauti zinazoishi Langas. Aliongeza kuwa huu ni mradi ambao hata akiondoka Eldoret, atakuwa anarudi kuuangalia.
Nyote mwaalikwa kushiriki kifedha, kimaombi na haswa kujitokeza siku hiyo na mwaombwa mnunue tishati za Matembezi ya Amani. Matembezi yenyewe yanajulikana kama “Mimi ni mwanzilishi wa Amani” na maudhui yake ni Amani Chaguo langu, Jamii moja Taifa moja. Kumbuka ni tarehe 29 mwezi huu.
☺Cheuo☺
Jumapili iliyopita kaka James Wesonga aliwashangaza waumini wengi alipovalia suti, na sio suti tu, bali ilikuwa ni suti ya vipande vitatu (3 piece). Suti yenyewe ilikuwa ya rangi ya jivu, shati nyeupe pe pe pe, viatu vyeusi na tai nono ya samawati. Wesonga anajulikana sana kwa kuvalia tishati hata wakati anapohubiri.
 Wengi waliomkaribia na waliokuwa mbali walionyesha mshangao wao, kumuona tanashati kiasi cha kudhaniwa anaelekea harusini au uwanja wa ndege, kumlaki John Piper. Kinyume na matarajio ya Kanisa FM, kaka Wesonga hakutoa vifungu vyovyote kuhusiana na mavazi yake ya siku hiyo. Wesonga ni maarufu kwa kuakifisha mazungumzo yake na vifungu kochokocho vya Bibilia.
Gatuzi la Timna, Ufilisti. Maelfu ya ekari za ngano ya Wafilisti yaliteketezwa na moto mkubwa huko Timna. Kwa mujibu wa mkuu wa Polisi wa gatuzi hilo, hicho kilikuwa ni kitendo cha kulipiza kisasi baada ya mja kusalitiwa na mkewe. Tumebaini kuwa mwanaume mmoja anayejulikana kama Samsoni alienda, akakamaata mamia ya mbweha, kisha akawafunga wawili kwa wawili katika mikia yao. Halafu akatwaa vienge vya moto na kuvitita mikiani. Baada ya hayo, aliwaachia mbweha hao kati ya ngano ya Wafilisti.
 Moto huo uliteketeza matita na ngano hata na mashamba ya mizeituni. Bado haijadhihirika ni mbinu gani aliyoitumia kuwanasa mbweha hao wote. Hiyo ni ripoti kama ilivyotumwa kwa vyombo vya habari kutoka kitabu cha Waamuzi 15:1-6.
KURUNZI MICHEZONI
Bingwa wa dunia wa uvuvi, Simoni Petro, hapo jana nusura afe maji. Petro alikuwa akishindana na Yesu katika uogeleaji mtindo wa Kutembea juu ya maji. Mwanzo Petro na timu yake walikuwa wameogopa Yesu huku wakisema ni kivuli, lakini Yesu alipowazungumzia Petro akawa na hamu ya kutembea juu ya bahari, pengine alitaka dhahabu nyingine ya Olimpiki.
 Hata hivyo aliona upepo na akahofia na akaanza kuzama. Hapo ndipo Yesu alipomnyoshea mkono na kumuokoa hadi katika mashua iliyokuwa karibu; huku akimuonya dhidi ya kuwa na imani haba. Haya yalifanyika huko Yerusalemu na ni kwa hisani ya chumba cha habari njema cha Mathayo 14:22-36.
 Kwingineko timu ya wapiga mbizi ya Israeli, iliipiku ile ya Misri katika uogeleaji wa shamu. Mkufunzi wa timu hio Bw. Musa aliwaongoza wenzake kutwaa ushindi huo hadi ng’ambo ya pili ya shamu. Kutokana na uzoefu wao wa kuogelea katika vidimbwi, Wanamisri walizama fyu na kufa maji kwani hawangemudu kasi ya mawimbi. Shirika la Uogeleaji halijatoa habari yoyote kuhusiana na miili ya Wamisri waliozama.
Aliyekuwa mchezaji wa Pharisee Rangers, Yuda Iskariote alijitia kitanzi baada ya kupigwa marufuku ya kushiriki dimba la kuingia mbinguni. Haya yalitokea baada ya kumchezea vibaya nahodha wa Christian United, Yesu Kristo.
Kwa mujibu wa Shirika la soka ya kuingia mbinguni, mchezaji huyo alipatikana na kosa lingine la kuhamia klabu kingine bila kuzingatia kanuni za uhamisho. Ilidhihirika kwamba Yuda, anayeechezea nambari 12 mgongoni, alinunuliwa kwa pauni thelathini siku moja kabla ya mchuano huo. Hata hivyo, yote ni kwa timizo ya mijumbe ya manabii.
Mwelekezi wetu anatuarifu kuwa wakati umetutia mikatale. Basi hatuna budi ila kutamatishia hapo. Asanti kwa kutupa masikio na makini yako. Tumekuwa wasimulizi wako... Tunawaacha na maneno ya maudhui ya Wafilipi 1:27 (a) “Lakini mwenendo wenu na uwe kama inavyopasa injili ya Kristo.” Barikiwa. 
                                                MWISHO
(Imetayarishwa na King’ori Wangechi na Wilson S. Muyanzi. Tuliisoma naye Beatrice Marori)