Monday 17 September 2012

KURUNZI YA KANISA FM 7



  15.09.2012
KURUNZI YA KANISA FM
“Njooni sasa, tutafakari pamoja.” Asema Bwana. Hayo ni maneno yake nabii Isaya. Yanatoka Isaya 1:18, na ndiyo maudhui ya Wikendi hii ya Washiriki. Ni wito wake Mungu ili tutoke dhambini na tumrejelee. Mengi tunayo kutoka gatuzi la Uasin Gishu na nje ya nchi, lakini kwanza tuvipate vimulimuli.
Ø Tutamulika Misheni ya Chuoni mwaka wa 2013...
Ø Tutakueleza kuhusu suti ya Wesonga...
Ø ... Na Michezoni tutamulika Uogeleaji.
Moja kwa moja kutoka Jumba la Inspiration House, barabara ya Biblical Avenue, hii ni Kurunzi Ya Kanisa FM. Karibu tukutaarifu kitimilifu, mimi ni King’ori Wangechi.
KURUNZI TIMILIFU
Hii ni wikendi ya kipekee ambayo tunajiunga na washiriki. Hawa ni waliokamilisha masomo yao, na huduma mbalimbali miaka iliyopita hapa chuoni na kanisani mtawalia. Ni wikendi iliyojaa shughuli tele zinazowahusisha washirika na washiriki. Furaha nyingi imeonekana nyusoni mwa wote. Hata hivyo, wikendi hii ya washiriki inaletwa kwenu kwa hisani ya Misheni ya Chuoni (Varsity Mission 2013).
Misheni ya Chuoni ni mpango unaotekelezwa kila baada ya miaka mitatu. Misheni hii ni ya kuwahubiria wote walio ndani na nje ya chuo. Ni mpango utakaofanyika mapema mwakani. Misheni yenyewe itajumuisha shughuli kama mikutano ya kufufua, siku ya mazingira, siku ya kunadhifishwa kwa kila mtu bila malipo, semina na nyimbo za sifa na pambio. Wahubiri na waimbaji wanaotambulika kitaifa na kimataifa wataalikwa, kushiriki. Nyote mwaalikwa ili tuanze kuhubiri Yerusalemu yetu iliyo chuo kikuu cha Moi. Hapo tutakuwa tumetimiza matakwa yake mwokozi kama yalivyo katika Luka 24:47,
“Na kwamba mataifa yote watahubiriwa kwa jina lake habari ya toba na ondoleo la dhambi kuanza tangu Yerusalemu.”
Misheni ya mwaka ujao ni tofauti na ingine yoyote. Hii imeandaa matembezi ya Amani huko Langas mjini Eldoret.
Matembezi hayo yatafanyika tarehe 29 Septemba mwaka huu. Yatafanyika vijijini vya Kisumu Ndogo, Yamumbi, Kasarani na Kahuruko. Hizi ni sehemu ambazo ziliathiriwa zaidi na ghasia za baada ya uchaguzi uliopita. Kamati andalizi ya Misheni ya chuoni ikaona ni hekima kuwa na matembezi ya Amani.
 Pauline Kachinja, mwenyekiti wa kamati andalizi ya matembezi ya Amani alinukuliwa na kanisa FM akisema kuwa sio matembezi ya siku moja tu, halafu mambo yawe basi, bali ni mpango unaonuiwa kuendelea na lengo lake ni kudumisha amani kati ya kabila tofauti zinazoishi Langas. Aliongeza kuwa huu ni mradi ambao hata akiondoka Eldoret, atakuwa anarudi kuuangalia.
Nyote mwaalikwa kushiriki kifedha, kimaombi na haswa kujitokeza siku hiyo na mwaombwa mnunue tishati za Matembezi ya Amani. Matembezi yenyewe yanajulikana kama “Mimi ni mwanzilishi wa Amani” na maudhui yake ni Amani Chaguo langu, Jamii moja Taifa moja. Kumbuka ni tarehe 29 mwezi huu.
☺Cheuo☺
Jumapili iliyopita kaka James Wesonga aliwashangaza waumini wengi alipovalia suti, na sio suti tu, bali ilikuwa ni suti ya vipande vitatu (3 piece). Suti yenyewe ilikuwa ya rangi ya jivu, shati nyeupe pe pe pe, viatu vyeusi na tai nono ya samawati. Wesonga anajulikana sana kwa kuvalia tishati hata wakati anapohubiri.
 Wengi waliomkaribia na waliokuwa mbali walionyesha mshangao wao, kumuona tanashati kiasi cha kudhaniwa anaelekea harusini au uwanja wa ndege, kumlaki John Piper. Kinyume na matarajio ya Kanisa FM, kaka Wesonga hakutoa vifungu vyovyote kuhusiana na mavazi yake ya siku hiyo. Wesonga ni maarufu kwa kuakifisha mazungumzo yake na vifungu kochokocho vya Bibilia.
Gatuzi la Timna, Ufilisti. Maelfu ya ekari za ngano ya Wafilisti yaliteketezwa na moto mkubwa huko Timna. Kwa mujibu wa mkuu wa Polisi wa gatuzi hilo, hicho kilikuwa ni kitendo cha kulipiza kisasi baada ya mja kusalitiwa na mkewe. Tumebaini kuwa mwanaume mmoja anayejulikana kama Samsoni alienda, akakamaata mamia ya mbweha, kisha akawafunga wawili kwa wawili katika mikia yao. Halafu akatwaa vienge vya moto na kuvitita mikiani. Baada ya hayo, aliwaachia mbweha hao kati ya ngano ya Wafilisti.
 Moto huo uliteketeza matita na ngano hata na mashamba ya mizeituni. Bado haijadhihirika ni mbinu gani aliyoitumia kuwanasa mbweha hao wote. Hiyo ni ripoti kama ilivyotumwa kwa vyombo vya habari kutoka kitabu cha Waamuzi 15:1-6.
KURUNZI MICHEZONI
Bingwa wa dunia wa uvuvi, Simoni Petro, hapo jana nusura afe maji. Petro alikuwa akishindana na Yesu katika uogeleaji mtindo wa Kutembea juu ya maji. Mwanzo Petro na timu yake walikuwa wameogopa Yesu huku wakisema ni kivuli, lakini Yesu alipowazungumzia Petro akawa na hamu ya kutembea juu ya bahari, pengine alitaka dhahabu nyingine ya Olimpiki.
 Hata hivyo aliona upepo na akahofia na akaanza kuzama. Hapo ndipo Yesu alipomnyoshea mkono na kumuokoa hadi katika mashua iliyokuwa karibu; huku akimuonya dhidi ya kuwa na imani haba. Haya yalifanyika huko Yerusalemu na ni kwa hisani ya chumba cha habari njema cha Mathayo 14:22-36.
 Kwingineko timu ya wapiga mbizi ya Israeli, iliipiku ile ya Misri katika uogeleaji wa shamu. Mkufunzi wa timu hio Bw. Musa aliwaongoza wenzake kutwaa ushindi huo hadi ng’ambo ya pili ya shamu. Kutokana na uzoefu wao wa kuogelea katika vidimbwi, Wanamisri walizama fyu na kufa maji kwani hawangemudu kasi ya mawimbi. Shirika la Uogeleaji halijatoa habari yoyote kuhusiana na miili ya Wamisri waliozama.
Aliyekuwa mchezaji wa Pharisee Rangers, Yuda Iskariote alijitia kitanzi baada ya kupigwa marufuku ya kushiriki dimba la kuingia mbinguni. Haya yalitokea baada ya kumchezea vibaya nahodha wa Christian United, Yesu Kristo.
Kwa mujibu wa Shirika la soka ya kuingia mbinguni, mchezaji huyo alipatikana na kosa lingine la kuhamia klabu kingine bila kuzingatia kanuni za uhamisho. Ilidhihirika kwamba Yuda, anayeechezea nambari 12 mgongoni, alinunuliwa kwa pauni thelathini siku moja kabla ya mchuano huo. Hata hivyo, yote ni kwa timizo ya mijumbe ya manabii.
Mwelekezi wetu anatuarifu kuwa wakati umetutia mikatale. Basi hatuna budi ila kutamatishia hapo. Asanti kwa kutupa masikio na makini yako. Tumekuwa wasimulizi wako... Tunawaacha na maneno ya maudhui ya Wafilipi 1:27 (a) “Lakini mwenendo wenu na uwe kama inavyopasa injili ya Kristo.” Barikiwa. 
                                                MWISHO
(Imetayarishwa na King’ori Wangechi na Wilson S. Muyanzi. Tuliisoma naye Beatrice Marori)

Wednesday 23 May 2012

KURUNZI YA KANISA FM 6


KURUNZI YA KANISA FM
Mengi ninayo kutoka gatuzi la Yerusalemu na vilevile kutoka kitabu cha Matendo ya Mitume. Lakini kwanza tuvipate vimulimuli.
-          Ufisadi waua mja na bibiye...
-          Hotuba ya Paulo...
-          Na nitakueleza ni nani aliyeachiliwa na ni nani aliyeshikwa na mahakama ya  kimataifa.
Hujambo na karibu kwa Kurunzi mimi ni Paul King’ori.
KURUNZI TIMILIFU
Nchi nyingi zimekuwa zikibwatika kwa sababu ya ufisadi. Habari za kusikitisha ni kwamba ufisadi ulipenya hadi kanisani kwa mja mmoja huko Yerusalemu. Mwanaume huyo anayejulikana kama Anania aliuza kipande cha shamba lake lakini akamua kuficha baadhi ya thamani ya mauzo. Kulingana na vile tulivyoarifiwa, Anania alipeleka fedha kwa kamati iliyokuwa ikishughulikia thamani zilizokuwa zikitolewa pale kanisani. Alipoulizwa kama hiyo ndiyo ilikuwa thamani yote alijibu ndiyo. Alikuwa amemghilibu Roho Mtakatifu. Alianguka na kukata roho papo hapo.
  Mwandishi wetu alipata habari kuwa  baada ya saa tatu mkewe yaani Safira alitia habta ya kanisani. Alipoulizwa na mwenyekiti wa kamati, Petero, alijibu kama mumewe. Ghafula bin vuu akaanguka na kufariki. Hayo yakawa malipo ya ufisadi. Chambilecho ya Biblia malipo ya dhambi ni kifo.
  Mwezi wa sita ndio  Dr. Martin Luther King Junior  alitoa hotuba maarufu ya kutotumia fujo katika chuo kikuu cha California. Kwingineko, Mtume Paulo ametoa hotuba maruufu ya maisha katika Kristo. Katika waraka aliouandikia Waefeso nambari ya usajili 4:26, anawashauri na kuwashawishi watende wema. Kinaya ni kuwa anawambia wawe na hasira, ila wasitende dhambi, jua lisichue kama bado na uchungu wao bado hujawatoka. Mwizi asiibe tena bali atende kazi nzuri kwa mikono yake mwenyewe. Halikadhalika, neno lililo ovu lisitoke vinywani mwao bali njema la kumfaa msikilizaji. Toeni maneno ya kuleta neema kwa wasikilizaji wenu. Wasiwe na uchungu, kelele au matukano. Yote ni tisa, la kumi, alisema wawe na huruma na wasahemeane kama Mungu alivyowasamehe  wao katika Kristo.  
   Hivi karibuni Kenya kulifanyika uteuzi wa viongozi wa idara ya mahakama. Kwingineko Yerusalemu, kumefanyika uteuzi wa aina yake. Stefano, Filipo,Prokoro, Nikanoni, Timoni, Paremena na Nikolau waliteuliwa ili kuunda jopokazi la kugawa fedha za msaada. Fedha hizi zilikuwa za kila siku kwa wajane. Haya yalitokea baada ya manung’uniko kuzuka kuwa wajane wa Kiebrania walikuwa wakisahaulika na wale wa Kiyunanikupewa fedha. Jopokazi hili lilipendeza machoni mwa kila mtu na neno la Mungu likaenea kama moto wa nyasi jangwani.

  KURUNZI KIMATAIFA
Maajabu hayataisha duniani. hapo jana binadamu walimpeleka Mwokozi wao, Yesu katika mahakama ya kimataifa. Walimkahifu kwa kudai kuwa yeye ni mwans\a wa Mungu. Ole wao! Jaji mkuu Pilato alimsomea Yesu mshtaka naye hakukana. Huko nje halaiki iliyokuwa imekusanyika huku ikipiga makelele, iliitisha Baraba baada ya Pilato kusema kuwa hamna ushahidi wa kutosha kumhukumu Yesu.
 Jaji hakuwa na lakufanya ila kunawa mikono, ishara kuwa damu ya Yesu haikuwa mikononi mwake. Tanzia ilikuwa kusulubiwa kwa Yesu. Faraja ikawa kufufuka baada ya siku tatu. Bwana apewe sifa. Mathayo 27.
KURUNZI MICHEZONI
Hapo jana mchezaji mashuhuri wa Tenisi Daudi alinyakua ushindi dhidi ya Mfilisti. Daudi aliyemshinda Goliathi kwa pointi 70-02, alijishindia taji la mchezaji bora duniani. Daudi sasa ameshikilia rekodi ya mchezaji mchanga mno kumshinda bingwa mtetezi wa Wafilisti. Daudi alipata ushindi huo baada ya kumuua Goliathi aliyekuwa akiwabeza wana wa Israeli kila uchao. Kutoka Kanisa FM, twampongeza Daudi na sifa zimwendee Mungu wa Isaka na Yakobo.
Kufikia hapo sina la ziada lakini endelea kutegea papa hapa kwa mengine mengi. Kwaheri na hadi wakati mwingine, mimi ni Paul King’ori.


Friday 4 May 2012

KURUNZI YA KANISA FM 5

KURUNZI YA KANISA FM
Wakati umenipa kibali ili niweze kukuletea habari jamali. Asanti sana kwa kujiunga nami nikikumulikia yaliyojiri kwa ijili. Lakini kwanza kawaida yetu ni kuvipata vimulimuli. 

VIMULIMULI
- Kinyesi kikavu chapika...
- Tutaangalia vita dhidi ya wanamgambo wa kiroho...
- na Michezoni Nehemia ashinda Tobia.
Hujambo na karibu mimi ni msimulizi wako Paul King’ori.

KURUNZI TIMILIFU

TAHADHARI: Mwelekezi wangu ananiarifu kuwa habari ifuatayo yaweza kuzua hisia zisizoridhisha hususan kama watafuna. Hata hivyo, ni ukweli mtupu... Nabii Ezekieli alipitia mateso ya aina yake huko Yerusalemu. Licha ya kuagizwa alalie kaure kwa siku 390, alikuwa anafungwa kwa kamba na Mungu ili asipinduke. Hii ni ishara ya vile Israeli watakavyofungwa utumwani. Hicho kilikuwa ni kionjo cha kiroja. Kilele chake kilikuwa cha kushangaza zaidi. Uhalisia ni kuwa kinyesi hutumika kuzalisha kawi. Aghalabu kawi yenyewe hutumika kupikia. Hata hivyo, mwenyezi Mungu alimweleza  Ezekieli apike kwa kinyesi cha binadamu. Ndiyo, cha binadamu. Mungu alimwamuru nabii huyo aoke mkate kutumia kinyesi kikavu. Haya yanaashiria uchafu wa dhambi za Yerusalemu. Ezekieli alipewa maelezo hayo na alipomlalamikia Mungu ya kuwa hajajichafua, Mungu alimhurumia na akamwambia aoke mkate wake kwa kinyesi cha ng’ombe kama mbadala. Hii ikawa ni ishara ya vile watakavyokula chakula kichafu kwa kuzidiwa na dhambi.
 Hayakuishia hapo. Aliambiwa anyoe ndevu na kichwa chake, kisha aigawe nywele aliyokata katika matuta. Alikuwa achome thuluthi moja, thuluthi nyingine aikate kwa upanga na nyingine aitawanye kwa upepo. Ya Mungu ni mengi na hiyo ni gharama ya dhambi dhidi yake. Ripoti hii ni kutoka Ezekieli 4 na 5.
Nyakati hizi za kisasa, nchi nyingi zimeshuhudia uhaba wa chakula. Hata hivyo gatuzi la Galilaya lilipata chakula cha msaada kutoka mbinguni (ama ukipenda Heaven For Galilee). Haya yalifuatia baada ya siku tatu za makali ya njaa. Makamu wa Rais aliwaonea huruma na kufanyia mikate mitano na samaki wawili mujiza. Bidhaa hizo zilikuwa chakula kingi mno cha thamani ya mamilioni ya pesa. Chakula hicho kiliishibisha halaikiya watu elfu tano! Kwa mujibu wa mmoja wa waliokula, aliyejitambulisha kama Mariko, alisema kilikuwa kitamu kupindukia na hata walibakisha vikapu kumi na viwili.
 Kinaya ni kuwa mujiza huu haukulipishwa kama miujiza mingi ya siku hizi. Kwa habari zaidi, tumia anwani ya mtandao ifuatayo. Holybible@ mark6.36-41.com

KURUNZI BIASHARA
  Huku shilingi ya Kenya ikiendelea kupoteza thamani kwa kasi, nchi ya Yerusaremu hivi karibuni huenda ikaanza kulia kivulini. Walakini lazima wananchi wafuate masharti ya Mwenyezi Mungu. Inawalazimu kutupilia mbali dhambi zao. Kulingana na kituo cha habari cha Isaya 55.1, Wanayerusaremu wataanza kula mikate na kunywa divai na maziwa bila kulipa hata thumni! Haya yatawezeshwa na Mungu mwenyewe ili wajue kuwa yeye ndiye Mungu Muumba na  kwamba yuamiliki kila kitu duniani. Wito wa usaidizi huo umepeanwa na Mola kupitia kwa msemaji wake nabii Isaya, huku akisema kuwa nia zenu si kama zake  wala mawazo yake kama yenu.

KURUNZI KIMATAIFA
   Hivi karibuni tumeshuhudia vita baina ya jeshi la Kenya na wanamgambo wa Al-Shabaab. Aghalabu vita hufanyika baina ya watu au nchi. Hii ni dhihirisho tosha kuwa vita ni vya aina nyingi. Uhalisia ni kuwa sisi Wakristo hatupigani vita vya kimwili ila twapigana vya Kiroho dhidi ya mwovu na ujanja wake. Hivyo basi ni muhimu kutumia silaha za kiroho, ili tushinde hivi vita. Baadhi ya silaha hizi ni; Mshipi wa Ukweli, kifuani tuvalie Utakatifu, viatu vya Ubashirina, ngao ya Imani, helmeti ya Wokovu na sime ya Neno la Mungu. Aidha tutumie gari la Maombi. Usaidizi wa Mungu utakaotokana na maombi ndio utakaokuwa mafuta ya magari yenu. Hii ni ripoti kutoka waraka wa Paulo kwa Waefeso 6:10-18.

KURUNZI MICHEZONI
   Katika michezo, timu ya Nehemia iliihemesha timu ya Tobia na Sanbalati huko Yerusalemu. Timu ya Sanbalati ilikuwa imekula njama ya kumchezea Nehemia vibaya,  kumjeruhi uwanjani na hatimaye kumuua. Ilifumbuliwa kuwa Sanbalati walikuwa wamepanga kumtega Nehemia uwanjani wa kujengea Ukuta. Hata hivyo Nehemia aliikwepa mikiki ya Tobia na kukataa kula mtama aliomwagiwa na akaendelea na kazi ya ujenzi wa ukuta. Hapo ndipo alipowafungia mabao saba kwa nunge kwani hawakumpata wamdhuru. Ripoti hiyo ya Nehemia 6 ndiyo inatukamilishia Kurunzi kwa sasa. Asanti kwa kunipa makini yako. Mungu akubariki na ukumbuke kumwombea mwenzako. Hadi wakati mwingine, mimi ni Paul King’ori. 




Saturday 24 March 2012

SHAIRI LA HARUSI

UA LANGU
Tumba langu tumba langu, lakunena ndilo sina.
Furaha yangu ja wingu, rohongu zidi kunona.
Meamua hiki chungu, kiwe shamba we hazina
Wanukia wavutia, ua langu umrembo.

Ulipokuwa wakua,  wengi litamani kwona.
Bawabu liweka ua,  dhuluma sije kwona.
Kaweka maji mbolea,  kivuli pasi kuguna.
Wanukia wavutia,  ua langu umrembo.

Umekua kwa madaha, wayafuata madili.
Leo mi nina furaha, eti twaenda manzili.
Nyumbetu iwe na raha, tusigawe mara mbili.
Wanukia wavutia, ua langu umrembo.

Harufuyo yanukia, kila nyuki yavutia.
Takulinda ja malkia, hakuna takufikia,
Penzi mia fil mia, hakiki hutaumia.
Wanukia wavutia, ua langu umrembo.

Umbo lako ni kiungo, rangi nayo yavutia.
Penzi lako kama tango, roho yangu yatulia.
Kikwona kwa mlango, macho siwezi zibia.
Wanukia wavutia, ua langu umrembo.

Nywele nayo maridadi, inang’ara kama mwezi.
Mwangaza pia wazidi, kwa macho ya chipukizi.
 Sauti yako waridi, yapendeza msikizi
Wanukia wavutia, ua langu umrembo.


Siku ya leo nakwoa, mahaba takupa tele.
Hakikisho hujanoa, hiyo pete kwa kidole.
Ndoa yetu naombea, twishi pamoja milele.
Wanukia wavutia, ua langu umrembo.

Nashukuru wakulima, kwa kutunza hili ua.
Ua mesimama wima, sababu ya kununua.
Ua hili ni lizima, pongezi kwa wakulima.
Wanukia wavutia, ua langu umrembo.

Na ya tisa ndiyo beti, kushukuru hi hadhira.
 Metulia kwenye viti, tazama pasi hasira.
Kishuhudia masharti, ya penzi hili duara.
Wanukia wavutia, ua langu umrembo.

Beti kumi nafikia, ua langu kisifia.
Si eti memalizia, wakati ndo wafifia.
Kuondoka naumia, kidosho kutomwimbia.
Wanukia wavutia, ua langu umrembo.


                                                                                       © PAUL KING’ORI,2009

SHAIRI LA UKIMWI

UKIMWI
Machozi yatudondoka, kwa hofu ya tulojua.
Hapa nami nagutuka, laiti wangelijua.
Mapenzi tulojitwika, kwao ja mchana jua.
Ukimwi hauna dawa, tiba wala kafaara.

Madawa twayanunua, nasi tunafilisika.
Hatuna kwa kufunua, mwelewa twasikitika.
Twajaribu kupanua, nasi tu twatilifika.
Ukimwi hauna dawa, tiba wala kafaara.

Watuacha bila mali, watoweka no wazazi.
Chakula hata hatuli, twatorokwa na pumzi.
Hatuwezi kaa tuli, na hatupati ng’o ndizi.
Ukimwi hauna dawa, tiba wala kafaara.

Maisha waliyapenda, si mengine tu anasa.
Walipenda lipya tunda, hata hilo kutomasa.
Wafurahia kutenda,vitendo vyaleta tasa.
Ukimwi hauna dawa, tiba wala kafaara.

Ole wao! Wenye neno,eti ukimwi ni homa.
Waungana yo mikono, kukataa moja boma.
Hawajui pigo nono, laja wana pokoroma.
Ukimwi hauna dawa, tiba wala kafaara.

Kahaba nao husema, haba hujaza kibaba.
Hata hivyo wanazama, kwa hukumu yake Baba.
Ijapokuwa natama, wana maradhi si haba.
Ukimwi hauna dawa, tiba wala kafaara.

Vijana nawasihini, tuwachane na madawa.
Nawaasa nyi jamani, hatutaupata wawa.
Tujitie vitabuni, tukatae kufanyiwa.
Ukimwi hauna dawa, tiba wala kafaara.

Nasi wale tuloachwa, twayahitaji mapenzi.
Iwe asubuhi au chwa, kuntu yasiwe ya tanzi.
Ili tuwe kama mchwa, pia tuwe na ulinzi.
Ukimwi hauna dawa, tiba wala kafaara.

Tuwafundishe yatima, tupate nazo baraka.
Tusivirekodi vima, nao watatajirika.
Hawatapata nadama, na hawatatamauka.
Ukimwi hauna dawa, tiba wala kafaara.

Tamati sasa nafika, nami natia nanga.
Natumai mewapachika, mawazo yakumpanga.
Yasije sahaulika, kwani yashinda upanga.
Ukimwi hauna dawa, tiba wala kafaara.
PAUL KING’ORI,CHUO KIKUU CHA MOI.

SHAIRI LA VIONGOZI

  VIONGOZI-Na Paul King'ori
Mmeipita mipaka, wazalendo waumia,
Wanazidiwa kumaka, huku pia wakilia,
Viongozi ninafoka, leo nawashambulia.
Viongozi ongozeni, kwa imani na mani

Mwadhulumu wazalendo, hamuijui na haki,
Mwawaogoza kwa fundo, ukweli nyi wazandiki,
Bayana hamna pendo, na hili nimehakiki.
Viongozi ongozeni, Kwa imani na amani.

Hongo na mnaitisha, dhahiri hamna soni,
Sikosei mwatadisha, maisha ni benibeni,
Nyinyi mwajifurahisha, wazalendo pasi kani.
Viongozi ongozeni, kwa imani na amani.

Uongozi wenu mwovu, sababu mwafuja mali,
Mwasema muwepevu, hamwishi kwa udhalili,
Mtanyakiwa kwa wavu, ufisadi ni majili.
Viongozi ongozeni, kwa imani na amani.

Mwatembelea waganga, ili mpate nyadhifa,
Nakuli kinaganaga, mwatuletea maafa,
Acheni kuleta janga, isikizeni kaifa.
Viongozi ongozeni, kwa imani na amani.


Kamwe hamna amani, migogoro mnazua,
Mmekuwa wapingani, amanini kutotua,
Mnachochea zogoni, kitali kutotatua,
Viongozi ongozeni, kwa imani na amani.

Leo hi mwanena mama, keshoye mwasema baba,
Mambo yaenda mrama, ukweli kenu ni haba,
Nyi chanzo cha hasama, yakini kosa haiba!
Viongozi ongozeni, kwa imani na amani.

Hitimisho nimefika, kalamu naweka chini,
Si uongo nimeng’aka, ukatili kaburini,
Acheni kuzururuka, gutukeni kwa halani.
Viongozi ongozeni, kwa imani na amani.

KURUNZI YA KANISA FM 4

KURUNZI YA KANISA FM
   “Kama mlivyompokea Kristo kama Bwana, basi nendeleeni kuishi ndani yake.” Hayo ni maneno yaliyosemwa na Paulo katika waraka wake kwa waumini wa Kolosia, S.L.P. Wakolosai 2:6. Kwa upande mwingine, ndiyo maudhui ya siku hii ambayo ni ya kusherehekea panda shuka za maisha ya chuo kikuu na kuwaaga wakongwe wetu. Hayawi hayawi hatimaye huwa. Hauchi hauchi hatimaye hukucha. Ilikucha siku moja wakajiunga na chuo kikuu na imekucha nyingine waondoke. Hawa ni wakongwe wetu. Mengi tunayo ya kuwamulikia lakini kwanza tuvipate vimulimuli.
VIMULIMULI
… Tutaangalia panda shuka za maisha ya wakongwe hapa chuoni…
…Tunazo habari za Oparesheni ya kulinda watakatifu…

... Na Divided Losers wazidiwa na masaibu.
KURUNZI TIMILIFU
  Waliingia chuoni mwaka wa 2007 na 2008. Hiyo ni miaka mitano na minne mtawalia iliyopita. Tunawazungumzia wakongwe tunaowapenda wanaofika hatima ya masomo yao ya hapa. Baadhi yao wakizungumza na Kanisa FM, walinukuu Biblia Zaburi 37:25 isemayo kuwa “Nilikuwa mchanga lakini sasa nimekomaa na sijaona mwaminifu akiwa ameachwa na Mungu.” Walisema kuwa watoto waliopewa wa kiroho hawajawahi omba chakula kwa uaminifu wake Mungu.
   Hata hivyo, walikumbuka kwa wepesi matatizo waliopitia wakiwa chuoni. Waliorodhesha migomo miwili. Mmoja hapo 2008 uliotokana na kupandishwa kwa nauli kupindukia, mgomo wenyewe ulisababisha vifo vya wanafunzi wawili. Wa pili ni mwaka jana uliohusisha shule ya Uhandisi wakati wa mitihani yao. Mitihani hiyo ilicheleweshwa hadi mwanzo wa mwaka huu. Wengine walisema wamekula magunia ya  sukuma mihula yote bila kubadilisha. Tatizo lingine kuu ni lile la kukosa malazi kila mwaka. Hili ni tatizo walilolikuta, na inaonekana ya kuwa wataliacha kama halijapata suluhisho. Ole wenu mnaobakia chuoni!
 Matatizo hayakuishia hapo, ukosefu wa fedha, kazi nyingi za ziada baada ya wahadhiri wakati mwingine kususia mihadhara na kukimbia mwishoni wa muhula na ukosefu wa wakati kwa pilkapilka  za hapa na pale.
 Hata hivyo, sio matatizo pekee waliokumbana nayo. Rika hili liliweza kushuhudia mengi ya kuonewa fahari. Injili iliyonoga katika chuo kikuu cha Moi almaarufu Varsity Mission 2010 pia ni swala la kuangaziwa kwani lilipata ufanisi mkubwa. Hii ni kutokana na ukombozi wa nyoyo na kubadilisha maisha ya watu wengi. Tukio kama hili linatarajiwa hapo mwakani. Halikadhalika, baadhi yao wameshiriki katika ubashirina huko Turkana unaojulikana kama Tri-Annual Mission. Mwisho wa mwaka jana, walihudhuria kwa wingi kongamano la Commision 2011. Hongera nyote mlioshiriki kwa hali na mali.
  Kwingineko waziri wa mashauri na mipango maalumu ya Kiroho Daktari Isaya akihutubia mkutano wa hadhara alinukuliwa akisema kuwa Mungu wetu ni wa maajabu mno. Huku akitoa mfano alisema kuwa Mungu huweza kunena kuhusu tamati ya jambo fulani akiwa ameshika asili yake. Aliongeza kuwa Mungu huhakikisha kuwa neno lolote lake litaishi milele na litatekeleza wajibu wowote ambao limetengewa kufanya. Ujumbe huu umetoka Isaya 46:8-11. Na kwa hivyo wanaomtumainia bwana watabarikiwa adui wapende wasipende.
--CHEUO--
KURUNZI KIMATAIFA
  Ndege ya kivita aina ya Drone imewarushia makombora mazito wafuasi wa kundi haramu la shetani. Hii ni kutokana na juhudi ya Oparesheni ya kulinda watakatifu ambayo imeingia siku yake ya miaka mingi. Majeshi  ya watakatifu wakiongozwa na Amiri jeshi mkuu ambaye ni Yesu Kristo lilichukuwa mwelekekeo mpya baada ya kundi hilo haramu kuoenekana  kufanya uhalifu mara kwa mara dhidi ya walokole. Ibilisi na kundi lake sasa limeachwa bila makao, njaa na kiu hali iliyopelekea wao kuhangaika duniani almaarufu kama World Tarmacking Network, la kufurahisha ni kuwa, hakuna matumaini.
  Kwingineko meli aina ya MV spirit imewateka nyara maharamia wengine wa kundi lilo hilo ambalo kwa sasa wanasubiri kusikizwa kwa kesi yao. Kwa kuwa mahakama ya kimataifa imeonekana haitaweza kuisikiza kesi hiyo, basi bila shaka watafikishwa kwenye mahakama ya Mbinguni. Hii imezua mtafaruku na mahangaiko kati ya wafuasi wengine. Kutokana na hali hii, kituo cha utangazaji cha Kanisa kinaomba kwa dharura injili na maombi kwa kundi hilo ili kuweza kukombolewa.
  Kesi ambayo haikupewa nafasi abadan katan ya kukata rufaa, iliyomkabili aliyekuwa wakati mmoja malaika mkuu aliyeachishwa kazi yake yenye ustaha mkubwa iliamuliwa mara moja. Kwenye uamuzi wake, jaji mkuu mwenye neema kubwa kubwa na ndogo ndogo tena mwenye hekima alimmwagisha unga malaika huyo kwa utovu wa nidhamu ya kutaka kuongezwa madaraka ili kutoshana na bosi wake. Yamkini alitaka kuienzi dunia bila adhari ya kuwa njia panda zilimshinda fisi.
KURUNZI MICHEZONI
  Kwa mujibu wa ripota wetu ambaye ni mwinjilisti Paulo, kinyang’anyiro kati ya malaika huyo ambaye sasa ana jina la kuogofya, ambalo ni shetani, na watakatifu bado inaendelea katika dakika zake za mwisho mwisho almaarufu dakika za ziada. Madhumuni ya kinyang’anyiro hicho ni kujizolea wafuasi wengi. Tahadhari kulingana na ripota wetu ni kuwa mtu yeyote akishawishika kufuata itikadi na mienendo ya ibilisi huyo basi bila shaka atatupwa pamoja na bosi wake katika ziwa la moto. Lakini afueni ni kuwa akiungama na kukiri dhambi zake basi bila shaka atasamehewa na mabaki ya akaunti yake ya M-Dhambi kubakia sufuri bin hamna.
  Hatimaye, mashabiki wengi wanayeunga mkono kwa dhati malaika mtakatifu wameonekana wakiimba nyimbo za kumtukuza na kumuenzi kocha wao ambaye ni Mungu mwenyewe kwa furaha kwani wameamini kwa nyoyo zao kuwa ushindi ni upande wao. Hii imeshuhudiwa katika maeneo mengi humu duniani kama vile katika Muungano wa Wakristo wa Chuo Kikuu Cha Moi, katika ibada ya leo ya kuwaaga wakongwe wao. Kwa upande mwingine, timu ya Divided Losers ikiongozwa na kocha wao, shetani imeonekana ikilemewa kwani kila sekunde, kuna kubadili wachezaji,mahangaiko, kukosa kuelewana, kulaumiana na hata kurushiana makonde mazito mazito, wenyewe kwa wenyewe wakiwa hapa duniani. 
Kwa hayo tunahitimisha Kurunzi lakini jiunge nasi wakati mwingine ili tumulike mengine. 
Nakutakia wakati usio na kero au kerezo. Ni mimi mwandishi wako Paul King'ori.
Imetayarishwa na Theorry Nahashown-(theuristheory@yahoo.com)na Paul King’ori-(wpaulkingori@yahoo.com).