15.09.2012
|
“Njooni sasa, tutafakari pamoja.” Asema
Bwana. Hayo ni maneno yake nabii Isaya. Yanatoka Isaya 1:18, na ndiyo maudhui
ya Wikendi hii ya Washiriki. Ni wito wake Mungu ili tutoke dhambini na
tumrejelee. Mengi tunayo kutoka gatuzi la Uasin Gishu na nje ya nchi, lakini
kwanza tuvipate vimulimuli.
Ø
Tutamulika
Misheni ya Chuoni mwaka wa 2013...
Ø
Tutakueleza
kuhusu suti ya Wesonga...
Ø
...
Na Michezoni tutamulika Uogeleaji.
Moja kwa moja kutoka Jumba la Inspiration
House, barabara ya Biblical Avenue, hii ni Kurunzi Ya Kanisa FM. Karibu
tukutaarifu kitimilifu, mimi ni King’ori Wangechi.
KURUNZI
TIMILIFU
Hii ni wikendi ya kipekee ambayo
tunajiunga na washiriki. Hawa ni waliokamilisha masomo yao, na huduma
mbalimbali miaka iliyopita hapa chuoni na kanisani mtawalia. Ni wikendi
iliyojaa shughuli tele zinazowahusisha washirika na washiriki. Furaha nyingi
imeonekana nyusoni mwa wote. Hata hivyo, wikendi hii ya washiriki inaletwa
kwenu kwa hisani ya Misheni ya Chuoni (Varsity Mission 2013).
Misheni ya Chuoni ni mpango unaotekelezwa
kila baada ya miaka mitatu. Misheni hii ni ya kuwahubiria wote walio ndani na
nje ya chuo. Ni mpango utakaofanyika mapema mwakani. Misheni yenyewe
itajumuisha shughuli kama mikutano ya kufufua, siku ya mazingira, siku ya
kunadhifishwa kwa kila mtu bila malipo, semina na nyimbo za sifa na pambio.
Wahubiri na waimbaji wanaotambulika kitaifa na kimataifa wataalikwa, kushiriki.
Nyote mwaalikwa ili tuanze kuhubiri Yerusalemu yetu iliyo chuo kikuu cha Moi.
Hapo tutakuwa tumetimiza matakwa yake mwokozi kama yalivyo katika Luka 24:47,
“Na
kwamba mataifa yote watahubiriwa kwa jina lake habari ya toba na ondoleo la
dhambi kuanza tangu Yerusalemu.”
Misheni ya mwaka ujao ni tofauti na
ingine yoyote. Hii imeandaa matembezi ya Amani huko Langas mjini Eldoret.
Matembezi hayo yatafanyika tarehe 29
Septemba mwaka huu. Yatafanyika vijijini vya Kisumu Ndogo, Yamumbi, Kasarani na
Kahuruko. Hizi ni sehemu ambazo ziliathiriwa zaidi na ghasia za baada ya
uchaguzi uliopita. Kamati andalizi ya Misheni ya chuoni ikaona ni hekima kuwa
na matembezi ya Amani.
Pauline Kachinja, mwenyekiti wa kamati
andalizi ya matembezi ya Amani alinukuliwa na kanisa FM akisema kuwa sio
matembezi ya siku moja tu, halafu mambo yawe basi, bali ni mpango unaonuiwa
kuendelea na lengo lake ni kudumisha amani kati ya kabila tofauti zinazoishi
Langas. Aliongeza kuwa huu ni mradi ambao hata akiondoka Eldoret, atakuwa
anarudi kuuangalia.
Nyote mwaalikwa kushiriki kifedha,
kimaombi na haswa kujitokeza siku hiyo na mwaombwa mnunue tishati za Matembezi
ya Amani. Matembezi yenyewe yanajulikana kama “Mimi ni mwanzilishi wa Amani” na
maudhui yake ni Amani Chaguo langu, Jamii moja Taifa moja. Kumbuka ni tarehe 29
mwezi huu.
☺Cheuo☺
Jumapili iliyopita kaka James Wesonga
aliwashangaza waumini wengi alipovalia suti, na sio suti tu, bali ilikuwa ni
suti ya vipande vitatu (3 piece). Suti yenyewe ilikuwa ya rangi ya jivu, shati
nyeupe pe pe pe, viatu vyeusi na tai nono ya samawati. Wesonga anajulikana sana
kwa kuvalia tishati hata wakati anapohubiri.
Wengi waliomkaribia na waliokuwa mbali
walionyesha mshangao wao, kumuona tanashati kiasi cha kudhaniwa anaelekea
harusini au uwanja wa ndege, kumlaki John Piper. Kinyume na matarajio ya Kanisa FM, kaka Wesonga hakutoa vifungu
vyovyote kuhusiana na mavazi yake ya siku hiyo. Wesonga ni maarufu kwa
kuakifisha mazungumzo yake na vifungu kochokocho vya Bibilia.
Gatuzi la Timna, Ufilisti. Maelfu ya
ekari za ngano ya Wafilisti yaliteketezwa na moto mkubwa huko Timna. Kwa mujibu
wa mkuu wa Polisi wa gatuzi hilo, hicho kilikuwa ni kitendo cha kulipiza kisasi
baada ya mja kusalitiwa na mkewe. Tumebaini kuwa mwanaume mmoja anayejulikana
kama Samsoni alienda, akakamaata mamia ya mbweha, kisha akawafunga wawili kwa
wawili katika mikia yao. Halafu akatwaa vienge vya moto na kuvitita mikiani.
Baada ya hayo, aliwaachia mbweha hao kati ya ngano ya Wafilisti.
Moto huo uliteketeza matita na ngano hata na
mashamba ya mizeituni. Bado haijadhihirika ni mbinu gani aliyoitumia kuwanasa
mbweha hao wote. Hiyo ni ripoti kama ilivyotumwa kwa vyombo vya habari kutoka
kitabu cha Waamuzi 15:1-6.
KURUNZI
MICHEZONI
Bingwa wa dunia wa uvuvi, Simoni Petro,
hapo jana nusura afe maji. Petro alikuwa akishindana na Yesu katika uogeleaji
mtindo wa Kutembea juu ya maji. Mwanzo Petro na timu yake walikuwa wameogopa
Yesu huku wakisema ni kivuli, lakini Yesu alipowazungumzia Petro akawa na hamu
ya kutembea juu ya bahari, pengine alitaka dhahabu nyingine ya Olimpiki.
Hata hivyo aliona upepo na akahofia na akaanza
kuzama. Hapo ndipo Yesu alipomnyoshea mkono na kumuokoa hadi katika mashua
iliyokuwa karibu; huku akimuonya dhidi ya kuwa na imani haba. Haya yalifanyika
huko Yerusalemu na ni kwa hisani ya chumba cha habari njema cha Mathayo
14:22-36.
Kwingineko timu ya wapiga mbizi ya Israeli,
iliipiku ile ya Misri katika uogeleaji wa shamu. Mkufunzi wa timu hio Bw. Musa
aliwaongoza wenzake kutwaa ushindi huo hadi ng’ambo ya pili ya shamu. Kutokana
na uzoefu wao wa kuogelea katika vidimbwi, Wanamisri walizama fyu na kufa maji
kwani hawangemudu kasi ya mawimbi. Shirika la Uogeleaji halijatoa habari yoyote
kuhusiana na miili ya Wamisri waliozama.
Aliyekuwa mchezaji wa Pharisee Rangers, Yuda Iskariote
alijitia kitanzi baada ya kupigwa marufuku ya kushiriki dimba la kuingia
mbinguni. Haya yalitokea baada ya kumchezea vibaya nahodha wa Christian United, Yesu Kristo.
Kwa mujibu wa Shirika la soka ya kuingia
mbinguni, mchezaji huyo alipatikana na kosa lingine la kuhamia klabu kingine
bila kuzingatia kanuni za uhamisho. Ilidhihirika kwamba Yuda, anayeechezea
nambari 12 mgongoni, alinunuliwa kwa pauni thelathini siku moja kabla ya
mchuano huo. Hata hivyo, yote ni kwa timizo ya mijumbe ya manabii.
Mwelekezi wetu anatuarifu kuwa wakati
umetutia mikatale. Basi hatuna budi ila kutamatishia hapo. Asanti kwa kutupa
masikio na makini yako. Tumekuwa wasimulizi wako... Tunawaacha na maneno ya
maudhui ya Wafilipi 1:27 (a) “Lakini mwenendo wenu na uwe kama inavyopasa
injili ya Kristo.” Barikiwa.
MWISHO
(Imetayarishwa
na King’ori Wangechi na Wilson S. Muyanzi. Tuliisoma naye Beatrice Marori)