Saturday 24 March 2012

SHAIRI LA HARUSI

UA LANGU
Tumba langu tumba langu, lakunena ndilo sina.
Furaha yangu ja wingu, rohongu zidi kunona.
Meamua hiki chungu, kiwe shamba we hazina
Wanukia wavutia, ua langu umrembo.

Ulipokuwa wakua,  wengi litamani kwona.
Bawabu liweka ua,  dhuluma sije kwona.
Kaweka maji mbolea,  kivuli pasi kuguna.
Wanukia wavutia,  ua langu umrembo.

Umekua kwa madaha, wayafuata madili.
Leo mi nina furaha, eti twaenda manzili.
Nyumbetu iwe na raha, tusigawe mara mbili.
Wanukia wavutia, ua langu umrembo.

Harufuyo yanukia, kila nyuki yavutia.
Takulinda ja malkia, hakuna takufikia,
Penzi mia fil mia, hakiki hutaumia.
Wanukia wavutia, ua langu umrembo.

Umbo lako ni kiungo, rangi nayo yavutia.
Penzi lako kama tango, roho yangu yatulia.
Kikwona kwa mlango, macho siwezi zibia.
Wanukia wavutia, ua langu umrembo.

Nywele nayo maridadi, inang’ara kama mwezi.
Mwangaza pia wazidi, kwa macho ya chipukizi.
 Sauti yako waridi, yapendeza msikizi
Wanukia wavutia, ua langu umrembo.


Siku ya leo nakwoa, mahaba takupa tele.
Hakikisho hujanoa, hiyo pete kwa kidole.
Ndoa yetu naombea, twishi pamoja milele.
Wanukia wavutia, ua langu umrembo.

Nashukuru wakulima, kwa kutunza hili ua.
Ua mesimama wima, sababu ya kununua.
Ua hili ni lizima, pongezi kwa wakulima.
Wanukia wavutia, ua langu umrembo.

Na ya tisa ndiyo beti, kushukuru hi hadhira.
 Metulia kwenye viti, tazama pasi hasira.
Kishuhudia masharti, ya penzi hili duara.
Wanukia wavutia, ua langu umrembo.

Beti kumi nafikia, ua langu kisifia.
Si eti memalizia, wakati ndo wafifia.
Kuondoka naumia, kidosho kutomwimbia.
Wanukia wavutia, ua langu umrembo.


                                                                                       © PAUL KING’ORI,2009

SHAIRI LA UKIMWI

UKIMWI
Machozi yatudondoka, kwa hofu ya tulojua.
Hapa nami nagutuka, laiti wangelijua.
Mapenzi tulojitwika, kwao ja mchana jua.
Ukimwi hauna dawa, tiba wala kafaara.

Madawa twayanunua, nasi tunafilisika.
Hatuna kwa kufunua, mwelewa twasikitika.
Twajaribu kupanua, nasi tu twatilifika.
Ukimwi hauna dawa, tiba wala kafaara.

Watuacha bila mali, watoweka no wazazi.
Chakula hata hatuli, twatorokwa na pumzi.
Hatuwezi kaa tuli, na hatupati ng’o ndizi.
Ukimwi hauna dawa, tiba wala kafaara.

Maisha waliyapenda, si mengine tu anasa.
Walipenda lipya tunda, hata hilo kutomasa.
Wafurahia kutenda,vitendo vyaleta tasa.
Ukimwi hauna dawa, tiba wala kafaara.

Ole wao! Wenye neno,eti ukimwi ni homa.
Waungana yo mikono, kukataa moja boma.
Hawajui pigo nono, laja wana pokoroma.
Ukimwi hauna dawa, tiba wala kafaara.

Kahaba nao husema, haba hujaza kibaba.
Hata hivyo wanazama, kwa hukumu yake Baba.
Ijapokuwa natama, wana maradhi si haba.
Ukimwi hauna dawa, tiba wala kafaara.

Vijana nawasihini, tuwachane na madawa.
Nawaasa nyi jamani, hatutaupata wawa.
Tujitie vitabuni, tukatae kufanyiwa.
Ukimwi hauna dawa, tiba wala kafaara.

Nasi wale tuloachwa, twayahitaji mapenzi.
Iwe asubuhi au chwa, kuntu yasiwe ya tanzi.
Ili tuwe kama mchwa, pia tuwe na ulinzi.
Ukimwi hauna dawa, tiba wala kafaara.

Tuwafundishe yatima, tupate nazo baraka.
Tusivirekodi vima, nao watatajirika.
Hawatapata nadama, na hawatatamauka.
Ukimwi hauna dawa, tiba wala kafaara.

Tamati sasa nafika, nami natia nanga.
Natumai mewapachika, mawazo yakumpanga.
Yasije sahaulika, kwani yashinda upanga.
Ukimwi hauna dawa, tiba wala kafaara.
PAUL KING’ORI,CHUO KIKUU CHA MOI.

SHAIRI LA VIONGOZI

  VIONGOZI-Na Paul King'ori
Mmeipita mipaka, wazalendo waumia,
Wanazidiwa kumaka, huku pia wakilia,
Viongozi ninafoka, leo nawashambulia.
Viongozi ongozeni, kwa imani na mani

Mwadhulumu wazalendo, hamuijui na haki,
Mwawaogoza kwa fundo, ukweli nyi wazandiki,
Bayana hamna pendo, na hili nimehakiki.
Viongozi ongozeni, Kwa imani na amani.

Hongo na mnaitisha, dhahiri hamna soni,
Sikosei mwatadisha, maisha ni benibeni,
Nyinyi mwajifurahisha, wazalendo pasi kani.
Viongozi ongozeni, kwa imani na amani.

Uongozi wenu mwovu, sababu mwafuja mali,
Mwasema muwepevu, hamwishi kwa udhalili,
Mtanyakiwa kwa wavu, ufisadi ni majili.
Viongozi ongozeni, kwa imani na amani.

Mwatembelea waganga, ili mpate nyadhifa,
Nakuli kinaganaga, mwatuletea maafa,
Acheni kuleta janga, isikizeni kaifa.
Viongozi ongozeni, kwa imani na amani.


Kamwe hamna amani, migogoro mnazua,
Mmekuwa wapingani, amanini kutotua,
Mnachochea zogoni, kitali kutotatua,
Viongozi ongozeni, kwa imani na amani.

Leo hi mwanena mama, keshoye mwasema baba,
Mambo yaenda mrama, ukweli kenu ni haba,
Nyi chanzo cha hasama, yakini kosa haiba!
Viongozi ongozeni, kwa imani na amani.

Hitimisho nimefika, kalamu naweka chini,
Si uongo nimeng’aka, ukatili kaburini,
Acheni kuzururuka, gutukeni kwa halani.
Viongozi ongozeni, kwa imani na amani.

KURUNZI YA KANISA FM 4

KURUNZI YA KANISA FM
   “Kama mlivyompokea Kristo kama Bwana, basi nendeleeni kuishi ndani yake.” Hayo ni maneno yaliyosemwa na Paulo katika waraka wake kwa waumini wa Kolosia, S.L.P. Wakolosai 2:6. Kwa upande mwingine, ndiyo maudhui ya siku hii ambayo ni ya kusherehekea panda shuka za maisha ya chuo kikuu na kuwaaga wakongwe wetu. Hayawi hayawi hatimaye huwa. Hauchi hauchi hatimaye hukucha. Ilikucha siku moja wakajiunga na chuo kikuu na imekucha nyingine waondoke. Hawa ni wakongwe wetu. Mengi tunayo ya kuwamulikia lakini kwanza tuvipate vimulimuli.
VIMULIMULI
… Tutaangalia panda shuka za maisha ya wakongwe hapa chuoni…
…Tunazo habari za Oparesheni ya kulinda watakatifu…

... Na Divided Losers wazidiwa na masaibu.
KURUNZI TIMILIFU
  Waliingia chuoni mwaka wa 2007 na 2008. Hiyo ni miaka mitano na minne mtawalia iliyopita. Tunawazungumzia wakongwe tunaowapenda wanaofika hatima ya masomo yao ya hapa. Baadhi yao wakizungumza na Kanisa FM, walinukuu Biblia Zaburi 37:25 isemayo kuwa “Nilikuwa mchanga lakini sasa nimekomaa na sijaona mwaminifu akiwa ameachwa na Mungu.” Walisema kuwa watoto waliopewa wa kiroho hawajawahi omba chakula kwa uaminifu wake Mungu.
   Hata hivyo, walikumbuka kwa wepesi matatizo waliopitia wakiwa chuoni. Waliorodhesha migomo miwili. Mmoja hapo 2008 uliotokana na kupandishwa kwa nauli kupindukia, mgomo wenyewe ulisababisha vifo vya wanafunzi wawili. Wa pili ni mwaka jana uliohusisha shule ya Uhandisi wakati wa mitihani yao. Mitihani hiyo ilicheleweshwa hadi mwanzo wa mwaka huu. Wengine walisema wamekula magunia ya  sukuma mihula yote bila kubadilisha. Tatizo lingine kuu ni lile la kukosa malazi kila mwaka. Hili ni tatizo walilolikuta, na inaonekana ya kuwa wataliacha kama halijapata suluhisho. Ole wenu mnaobakia chuoni!
 Matatizo hayakuishia hapo, ukosefu wa fedha, kazi nyingi za ziada baada ya wahadhiri wakati mwingine kususia mihadhara na kukimbia mwishoni wa muhula na ukosefu wa wakati kwa pilkapilka  za hapa na pale.
 Hata hivyo, sio matatizo pekee waliokumbana nayo. Rika hili liliweza kushuhudia mengi ya kuonewa fahari. Injili iliyonoga katika chuo kikuu cha Moi almaarufu Varsity Mission 2010 pia ni swala la kuangaziwa kwani lilipata ufanisi mkubwa. Hii ni kutokana na ukombozi wa nyoyo na kubadilisha maisha ya watu wengi. Tukio kama hili linatarajiwa hapo mwakani. Halikadhalika, baadhi yao wameshiriki katika ubashirina huko Turkana unaojulikana kama Tri-Annual Mission. Mwisho wa mwaka jana, walihudhuria kwa wingi kongamano la Commision 2011. Hongera nyote mlioshiriki kwa hali na mali.
  Kwingineko waziri wa mashauri na mipango maalumu ya Kiroho Daktari Isaya akihutubia mkutano wa hadhara alinukuliwa akisema kuwa Mungu wetu ni wa maajabu mno. Huku akitoa mfano alisema kuwa Mungu huweza kunena kuhusu tamati ya jambo fulani akiwa ameshika asili yake. Aliongeza kuwa Mungu huhakikisha kuwa neno lolote lake litaishi milele na litatekeleza wajibu wowote ambao limetengewa kufanya. Ujumbe huu umetoka Isaya 46:8-11. Na kwa hivyo wanaomtumainia bwana watabarikiwa adui wapende wasipende.
--CHEUO--
KURUNZI KIMATAIFA
  Ndege ya kivita aina ya Drone imewarushia makombora mazito wafuasi wa kundi haramu la shetani. Hii ni kutokana na juhudi ya Oparesheni ya kulinda watakatifu ambayo imeingia siku yake ya miaka mingi. Majeshi  ya watakatifu wakiongozwa na Amiri jeshi mkuu ambaye ni Yesu Kristo lilichukuwa mwelekekeo mpya baada ya kundi hilo haramu kuoenekana  kufanya uhalifu mara kwa mara dhidi ya walokole. Ibilisi na kundi lake sasa limeachwa bila makao, njaa na kiu hali iliyopelekea wao kuhangaika duniani almaarufu kama World Tarmacking Network, la kufurahisha ni kuwa, hakuna matumaini.
  Kwingineko meli aina ya MV spirit imewateka nyara maharamia wengine wa kundi lilo hilo ambalo kwa sasa wanasubiri kusikizwa kwa kesi yao. Kwa kuwa mahakama ya kimataifa imeonekana haitaweza kuisikiza kesi hiyo, basi bila shaka watafikishwa kwenye mahakama ya Mbinguni. Hii imezua mtafaruku na mahangaiko kati ya wafuasi wengine. Kutokana na hali hii, kituo cha utangazaji cha Kanisa kinaomba kwa dharura injili na maombi kwa kundi hilo ili kuweza kukombolewa.
  Kesi ambayo haikupewa nafasi abadan katan ya kukata rufaa, iliyomkabili aliyekuwa wakati mmoja malaika mkuu aliyeachishwa kazi yake yenye ustaha mkubwa iliamuliwa mara moja. Kwenye uamuzi wake, jaji mkuu mwenye neema kubwa kubwa na ndogo ndogo tena mwenye hekima alimmwagisha unga malaika huyo kwa utovu wa nidhamu ya kutaka kuongezwa madaraka ili kutoshana na bosi wake. Yamkini alitaka kuienzi dunia bila adhari ya kuwa njia panda zilimshinda fisi.
KURUNZI MICHEZONI
  Kwa mujibu wa ripota wetu ambaye ni mwinjilisti Paulo, kinyang’anyiro kati ya malaika huyo ambaye sasa ana jina la kuogofya, ambalo ni shetani, na watakatifu bado inaendelea katika dakika zake za mwisho mwisho almaarufu dakika za ziada. Madhumuni ya kinyang’anyiro hicho ni kujizolea wafuasi wengi. Tahadhari kulingana na ripota wetu ni kuwa mtu yeyote akishawishika kufuata itikadi na mienendo ya ibilisi huyo basi bila shaka atatupwa pamoja na bosi wake katika ziwa la moto. Lakini afueni ni kuwa akiungama na kukiri dhambi zake basi bila shaka atasamehewa na mabaki ya akaunti yake ya M-Dhambi kubakia sufuri bin hamna.
  Hatimaye, mashabiki wengi wanayeunga mkono kwa dhati malaika mtakatifu wameonekana wakiimba nyimbo za kumtukuza na kumuenzi kocha wao ambaye ni Mungu mwenyewe kwa furaha kwani wameamini kwa nyoyo zao kuwa ushindi ni upande wao. Hii imeshuhudiwa katika maeneo mengi humu duniani kama vile katika Muungano wa Wakristo wa Chuo Kikuu Cha Moi, katika ibada ya leo ya kuwaaga wakongwe wao. Kwa upande mwingine, timu ya Divided Losers ikiongozwa na kocha wao, shetani imeonekana ikilemewa kwani kila sekunde, kuna kubadili wachezaji,mahangaiko, kukosa kuelewana, kulaumiana na hata kurushiana makonde mazito mazito, wenyewe kwa wenyewe wakiwa hapa duniani. 
Kwa hayo tunahitimisha Kurunzi lakini jiunge nasi wakati mwingine ili tumulike mengine. 
Nakutakia wakati usio na kero au kerezo. Ni mimi mwandishi wako Paul King'ori.
Imetayarishwa na Theorry Nahashown-(theuristheory@yahoo.com)na Paul King’ori-(wpaulkingori@yahoo.com).




KURUNZI YA KANISA FM...3


KURUNZI YA KANISA FM
  Misheni ni taashira ya zama za kale. Hata leo huendelea na matokeo yake ni ya kuridhisha na kuhuzunisha pia. Kufurahisha kwani watu hupewa matumaini ya maisha ya paradiso. Kuhuzunisha kwa sababu wengine hurudia hali zao za awali za kutenda dhambi na hivyo kufanya misheni kuzunguka tu… Mengi ninayo kutoka gatuzi la Yerusalemu na kwengine lakini kwanza tuvipate vimulimuli.
VIMULIMULI
-Yerusalemu waandamana wakiitisha rais…
-Ibada Moi sasa ni mbili…
-Huenda Yerusalemu isihitaji shilingi kufanya biashara.
Na nitakweleza yaliyojiri katika ligi ya Ukuta… Hujambo na karibu nikutaarifu, mimi ni Paul King’ori.
KURUNZI TIMILIFU
   Nchi kadhaa za Afrika zimekuwa zikipanga mapinduzi dhidi ya viongozi wao. Kwingineko Israeli wameanza kufanya maandamano huku wakiitisha kiongozi wanayemuona ili wafanane na majirani wao. Hiki ni kinyume cha sheria na kanuni walizopewa na Mungu. Alikuwa amewahakikishia kuwa yeye ndiye kiongozi au Mfalme wao, ingawa hawamuoni.
Hata hivyo, walijitetea na kusema kuwa wanafanya hivyo kwani wana wa Samweli wamekiuka maadili ya uongozi wa hekalu. Wamemkuta Samweli na kumwambia awatafutie mfalme. Walakini Samweli amesita na kuwaonya kuwa mfalme atawanyanyasa, lakini hawangesikia la mwidhini wala la mteka maji Mto Tana. Hivyo basi Samweli hakuwa na budi ila kuwapa Saulo, na kumtakasa akawa mfalme wa Israeli. Ama kwa kweli, mtoto akililia wembe, hata jembe msukumie. Ripoti ya Samweli wa Kwanza 8 na 9.
  Na huko Zarefathi, Israeli, Eliya aliendelea kufanya miujiza huku akimsaidia mjane mmoja kupata chakula wakati wa kiangazi, ila tu kwa ukarimu wa mjane huyo. Eliya aliyekuwa amewakwa na makali ya njaa, alimsihi mjane amtayarisie chakula lakini mjane akamwelezea kuwa hana chochote isipokuwa unga na mafuta kiasi mno.
  Mjane alimweleza kwamba alikuwa katika harakati za kutayarisha  chakula cha mwisho wale pamoja na mtoto wake kisha wafe njaa. Nabii Eliya alimwaahidi na kumtimizia kwani unga na mafuta hayakupungua mpaka ukame ukaisha. Hapa tunasihiwa kuwa tusivibane tulivyo navyo hata viwe vichache namna gani. Ripoti ya Wafalme wa kwanza 17:8-18.
  Yerusalemu. Yesu aliwakusanya wanafunzi wake halafu akawapa nguvu za kuzoa mashetani na kuponya ndwele. Hata hivyo, kwa vile kuugua si kufa lakini, ugonjwa ni suna, kufa ni faradhi, walitumwa kuwaauni watu katika maisha ya baada ya kifo. Wajumbe hao kumi na wawili, walipewa masharti, kutoingia kwa waliohitimu kama Wanasamaria. Ila wende kwa waliopotoka, watu wa Israeli. Jukumu lao lilikuwa ni kuhubiri ya kwamba ufalme wa mbinguni u karibu kama kesho. Waponye wanaougua, wafufue, waponye walio na shida ya ngozi na wazoe mashetani kote duniani. Baada ya hayo yote, waliagizwa kutolipisha muujiza wowote kwani walipokea bure, na bure wapeane. Mathayo 10.
Haya ni baadhi ya mambo yatakayofunzwa katika warsha ya 2011 maarufu kama Commission 2011. Warsha yenyewe itafanyika katika Chuo Kikuu Cha Kabarak kwanzia tarehe 28 Disemba 2011 hadi tarehe 3 Januari 2012. Kwa mujibu wa Nelius Wangari, ambaye anashughulikia usajili, alisema kuwa fedha zinazohitajika ni shilingi 4,900 tu!
 Hata hivyo elfu moja kati ya hizo nne ni ya sajili. Aidha, Wangari akiongea na Kanisa FM, alisema kuwa, unaweza kupata fomu ya kuchangisha pesa hizo, hivyo basi usiwe na shaka. Aliongezea kuwa pesa hizo hazilingani kamwe na thamani ya mafunzo utakayopata. Haya ni mambo utakayotumia hata maishani ya halafu. Usajili unakamilika mwisho wa mwezi huu. Pia utafunzwa jinsi ya kubashiri, yaani misheni. Je, utawachwa?
  Matukio ya hivi karibuni hapa kanisani ni kuongezeka kwa waumini. Haya yametokana na wainjilisti wa kanisa hili kujitolea mhanga na kueneza injili, karibu, mbali na kwa vyovyote vile. Waumini walitoka kila jumba na chumba na kufurika furi furi kwa ibada hadi nafasi za viti zikaadimika mno. Wengine walilazimika kuketi nje na wengine wakaamua kurudi vyumbani. Hizi ni baadhi ya sababu zilizomfanya aliyekuwa mwenyekiti, Bw. Timothy Kemboi na jopo lake kuketi kitako na kujadiliana la kufanya. Waumini walipewa fursa ya kutoa maoni yao pia.
   Asilimia kubwa ikaunga mkono dhana ya ibada mbili kila jumapili. Sasa hivi ninapopeperusha, waumini wanazo shukurani kemkem kwa uongozi wa kanisa kwa kujitolea na kuajibika katika huduma.
CHEUO…
KURUNZI BIASHARA
  Huku shilingi ya Kenya ikiendelea kupoteza thamani kwa kasi, nchi ya Yerusalemu hivi karibuni huenda ikaanza kulia kivulini. Walakini lazima wananchi wafuate masharti ya Mwenyezi Mungu. Inawalazimu kutupilia mbali dhambi zao. Kulingana na kituo cha habari cha Isaia 55:1, Wanayerusalemu wataanza kula mikate, kunywa divai na maziwa bila kulipa hata thumni? Haya yatawezeshwa na Mungu mwenyewe ili wajue kuwa yeye ndiye Mungu Muumba na kwamba yuamiliki kila kitu duniani. Wito wa usaidizi huo umepeanwa na Mola kupitia kwa msemaji wake nabii Isaia, huku akisema kuwa nia zenu si kama zake wala mawazo yake kama yenu.
KURUNZI MICHEZONI
  Katika michezo, timu ya Nehemia iliihemesha timu ya Tobia na Sanbalati huko Yerusalemu. Timu ya Sanbalati ilikuwa imekula njama ya kumchezea Nehemia vibaya na kumuua. Ilifumbuliwa kuwa Sanbalati walikuwa wamepanga kumtega Nehemia uwanjani wa kujengea ukuta. Hata hivyo Nehemia aliikwepa mikiki ya Tobia na kukataa kula mtama aliomwagiwa na akaendelea na kazi ya ujenzi wa ukuta. Hapo ndipo alipowafungia mabao nane kwa nunge kwani hawakumpata wamdhuru. Ripoti ya Nehemia 6.
 Na hapo ndipo tutakapozimia Kurunzi siku ya leo, kama kawaida ni furaha iliyoje kushikana mikono na kumulika pamoja. Hadi wakati mwingine nimekuwa wako Paul King’ori.

Thursday 22 March 2012

KURUNZI YA KANISA FM...2

HABARI YA KANISA FM
Asanti sana kwa kujiunga nasi tena tunapomulika  yaliyojiri katika nyanja za kiroho. Nina mengi niliyokwandalia leo lakini kawaida ni kama sheria… Vimulimuli kwanza.
VIMULIMULI
-Vijana wasiwe wavivu…
-Hakuna limshindalo Mola…
-Mchezaji Daudi aweka rekodi mpya ya Tenisi… na
-Wanafunzi watunukiwa.
Hujambo na karibu kwa habari timilifu. Mimi ni Paul King’ori.
HABARI TIMILIFU
   Waziri wa maswala ya vijana na Werevu Profesa Suleimani leo amewaasa vijana dhidi ya uvivu na ulegevu. Huku akipigia mfano wa shamba la mtu mvivu alisema shamba hilo hujawa na miiba na ua wake huwa umeanguka. Akizungumza na Kanisa FM Profesa Suleimani aliongeza kuwa watu wavivu huvamiwa na umaskini kama jambazi. Kwa habari zaidi tumia anwani ifaatayo ya mtandao Proverbs @ Bible. 24:30.co.ke Waziri alikuwa akihutubia mkutano wa hadhara katika ziara zake za magatuzi.
  HABARI KUTOKA BUNGE
   Mbunge maalumu malaika wa Mungu leo alimhimiza waziri wa injili Mheshimiwa Luka ajibu swali na azungumzie swala lalilozua utata katika katiba hususan wakati huu ambapo kunazo harakati za kuitekeleza katiba mpya.
Swali hilo lililo katika kitabu cha Sheria cha Mwanzo 18:14 linauliza “Je, kuna jambo ngumu zaidi kwa Mungu?”
Mheshimiwa Luka aliye pia ni mwenyekiti wa kamati ya Bunge ya Binguni ya Uenezaji wa Injili alisimama kwa idhini ya Spika na kulijibu swali hilo kwa kifupi lakini kwa uhalisi ufaao. Akirejelea ripoti aliyokuwa ameitoa hapo awali iliyojulikana kama ‘The Luke Report,’ iliyonukuliwa kutoka kitabu cha Luka 1:37 alisema kuwa hakuna jambo lisilowezekana na Mwenyezi Mungu. Hii ni Ripoti iliyonuiwa kuwapa motisha wale wote ambao hawajafanikiwa kufikia kiwango kihitajikacho ili watunukiwe, basi wasife moyo kamwe, watie bidii na wamtumainie Mungu.
KURUNZI MICHEZONI
Hapo jana mchezaji mashuhuri wa Tenisi Daudi alijinyakulia ushindi kwa mara ya Tano mfululizo dhidi ya Mfilisti. Daudi aliyemshinda Goliathi kwa pointi 70-02 alijishindia taji la mchezaji bora duniani. Daudi pia ndiye mchezaji mchanga mno kumshinda Bingwa mtetezi wa Waflisti, Goliathi. Daudi alipata ushindi baada ya kumuua Goliathi aliyekuwa akiwabeza wana wa Israeli kila uchao. Kutoka kanisa Fm tunampongeza Daudi na sifa zimwendee Mungu wa Isaka na Yakobo.
HALI YA ANGA
Leo hali ya anga imebadilika kidogo katika Shule ya Upili ya Kairo maanake kuna mchanganyiko wa rangi. Haya ni matokeo ya halaiki kubwa iliyohudhuria  na ni tofauti na ile rangi ambayo imezoa macho, yaani rangi ya sare nyekundu. Pia nyusi za joto zitakuwa juu kidogo kwa furaha ya wanafunzi kwa kutembelewa na wazazi na wageni wengine na la muhimu zaidi kutunukiwa.
Basi kwa watakaotunukiwa-Pongezi na Hongera nyingi kutoka Kanisa FM. Kwa wale hawajabahatika, kuna kesho utie bidii… Mwelekezi wangu ananiarifu kuwa wakati umenitia mikatale, sina budi kuondoka. Hadi siku nyingine, barikiwa. Mimi ni Paul King’ori.  

KURUNZI YA KANISA FM....1

Ifuatayo ni taarifa ya habari ya Kanisa FM moja kwa moja kutoka Biblical Avenue, Inspiration House. Lakini kwanza tupate vimulimuli;
VIMULIMULI:
Ziwa Lawa nchi kavu…
Vijana ni muhimu…
Timu ya Ayubu ya shinda nishani ya dhahabu… Na
Nyote mwaonywa.
Hujambo na karibu mimi ni msimulizi wako Paul King’ori.
Na habari timilifu ndio hii.
  Huku vitendo vya Ilahi vikizidi kunoga na kumakisha mno, hapo jana aliendelea kuwastajaabisha wazalendo  Waisraeli. Wana hao waliokuwa wamekosa imani na Mungu wao na pia kiongozi wao Mteule Musa, waligutuka kuona miujiza ya Mola. Mbele yao mlikuwa na ziwa jekundu na nyuma yao mlikuwa na jeshi la askari wa Firauni, chambilecho ukistaajabu ya Musa utayaona ya Firauni. Mola mwenye huruma tele aliligawa ziwa hilo mara mbili na wanawaisraeli wakapitia katikati kulikokuwa kumekauka kiasi cha kutoa vumbi. La kuhangaisha ni kuwa, Waisraeli walipopita wote ng’ambo ya pili, ziwa lilirudi pahala pake na wanajeshi wa Firauni wakazama fyu! Usisahau kuwa Waisraeli walikuwa salama salimini.
 Waziri wa mashauri ya vijana Profesa Kohelethu leo asubuhi, alitoa hotuba kutoka kitabu chake Mlango wa 2:13-14. Akizungumza na Kanisa FM alitueleza kuwa, vijana wanafaa kuwa na macho pajini mwa nyuso zao ili waweze kuona mbele na mbali, sio tu kwa maisha bali kwa maisha ya kiroho hususani ya kibinafsi.
   Kikundi kisicho cha serikali yaani (NGO) kinachotetea haki za vijana kimetoa habari ya kuwaasa vijana haswa wakati huu tunakaribia mwisho wa mwaka kwa hivyo sherehe mbalimbali. Kwa mujibu wa ripoti zilizotumwa katika vyumba vya habari, zilisema kuwa mwenyekiti wa kikundi hicho anayeitwa Mteule Suleimani, alisema kuwa maji ya kuibiwa huwa matamu na mkate wa sirini hupendeza, hivyo basi wajikinge na anasa zisizofaa. Pia alinukuliwa akisema kuwa njia za wavivu hujaa miiba lakini njia za watu wenye bidii huwa kama barabara nyororo. Kwa hii alimaanisha kuwa wajihusishe na mambo yatakayotoa ufanisi maishani. Hii ni ripoti iliyotoka kitabu cha Methali 9:17 na Methali 15:19.
HABARI ZAIDI
  Ni dhahiri shahiri kuwa Kanisa FM ipo ili kukujulisha mambo yanapoibuka kila kuchao. Habari zinazonifikia sasa hivi zinasema kuwa Bwana Yesu mwana wa pekee wa Mungu anatarajiwa kutua ulimwenguni hivi karibuni. Duru za kuaminika zimetuarifu kuwa kulingana na Yohana, Binguni ipo na pia kuna Ahera. Hii ni ripoti kutoka Ufunuo 22:20
KURUNZI MICHEZONI
  Klabu bingwa mtetezi wa kanisa cha Ufanisi kinachoongozwa na kinara hodari Mungu Mtakatifu leo asubuhi kiliichapa timu ya kocha mlalahoi shetani bao 7-0. Bao zote zilipeperushwa wavuni na mchezaji hodari na wakujitolea muhanga Ayubu aliyesaidiwa na Roho Mtakatifu. Bao hizo zilikuwa za ushindi mkumbwa maanake ziliiwezesha timu ya Ufanisi Football Club kuchukua nishani ya dhahabu. Ayubu alirudishiwa mali yake maradufu. Mchezo huo uliokuwa na wasiwasi baada ya kocha duni shetani kujaribu kumhonga refa kwa kumwambia Ayubu amlaani Mungu, kitendo ambacho kilimfanya shetani apewe kadi nyekundu yaani ‘Red Card’.
HALI YA ANGA
Leo jioni kutakuwa na utulivu wa mapenzi ya Mungu, Mwana na Roho Mtakatifu.
Hatimaye kutakuwa na joto jingi kutokana na neno litakalotolewa na mhubiri leo hii.
Naam kadi ya tamati nimefika. Nakutakia wakati murua mimi ni Paul King’ori.
Kumbuka kuwa: Tunaweza kufanya mambo yote kutokana na mwenye kutupa nguvu.

Saturday 10 March 2012

KURUNZI YA COMMISSION

KURUNZI YA KANISA FM
“ Huu ndio wito, kuwa mashahidi wa Kristo.
Tu wafanyikazi waaminifu. Tumejazwa nguvu na upendo.
Tumetumwa kote duniani.
Yesu nisaidie, Bwana nisaidie, kwa kuwa huu ndio wito.”
  Hiki ni kibwagizo cha wimbo wa maudhui ya Commision 2011. Wimbo wenyewe uliandikwa na Terry Nzaumi, kutoka Kenya Methodist University.
Mengi ninayo lakini kwanza tupate vimulimuli vya Kurunzi. 

VIMULIMULI
... Maelfu yakusanyika katika kongamano…
… Rais Mstaafu awashangaza wengi kwa kunukuu Biblia…
… Tamasha la mwaka mpya lawasha moto…
… na Wanamoi wajaa Kabarak.
Hujambo na karibu nikutaarifu kikamilifu. Mimi ni Paul King'ori.

KURUNZI TIMILIFU
   Jumatano ya tarehe 28 Disemba mwaka jana ilikuwa ni siku ya wajumbe kusafiri. Barabara zote, za Kenya na Afrika Mashariki zilielekea mji mtulivu na safi wa Nakuru, Chuo kikuu cha Kabarak. Chuo chenyewe kina mandhari ya kuvutia,tulivu na ina mijengo ya kisasa. Kwa mujibu wa habari tulizokusanya dakika chache baada ya kuwasili, zilisema kuwa wajumbe walianza kuingia Kabarak saa mbili asubuhi. Wajumbe walikuwa wametoka; Kenya, Uganda, Tanzania, Rwanda, Ethiopia, Sudan ya Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Malawi, Nigeria na Norway.
   Idadi iliyokuwako ni takribani elfu tatu mia tano. Usajili wa idadi hiyo kubwa ya wajumbe ulileta matatizo ya hapa na pale. Ilibidi usitishwe ili wajumbe wapate chajio na wamshukuru Mungu kwa safari njema. Usajili uliendelea hadi saa sita usiku, siku hiyo ya kwanza. Mathalan, kawaida ni kama sheria. Kuna wajumbe walikuwa wanaingia saa tatu za usiku.
   Siku ya pili, Rais mstaafu Daniel Toroitich arap Moi aliwasili, aliwakaribisha wajumbe na kufungua kongamano rasmi. Usisahau kuwa ndiye mdhamini mkuu wa chuo hicho. Usiudharau wembamba wa reli, gari la moshi hupita, alikuwa akinukuu vifungu vya Biblia na kuwaacha wajumbe wengine vinywa wazi.
   Baada ya idhini kutoka kwa mwenye nyumba, kongamano lilianza mara moja, huku Askofu David Oginde akizichambua changamoto za kusikiza. Umuhimu wa somo hili  kuanza ulikuwa kuwafungua wajumbe ili waweze kusikiza mengine yote yaliyofuatia.
   Kongamano lenyewe, lilikuwa la nane lililoandaliwa na Ushirika wa Miungano ya Wakristo wa Kenya, ukipenda, “FOCUS Kenya”. Kaulimbiu ya kongamano ilikuwa ni kutoka Yohana 20:21 isemayo, “Kama baba alivyonituma, nami nawapeleka ninyi.” Kisisitizi kikiwa “Tumeitwa tuwe mashahidi waaminifu.” Masomo yote yalizunguka kaulimbiu. Kwa hivyo tulifunzwa mengi kuhusu ubashirina au misheni.

~~~CHEUO~~~

   Wazungumzaji katika kongamano walikuwa ni Femi Adeleye kutoka Nigeria, Steve Maina aliye na huduma New Zealand, Dkt. Antonia Leonara van der Meer, kutoka Brazil,aliyekuwa mwanafunzi wa Chuo kikuu cha Moi, Peter Oyugi anayehudumu London, Uingereza,Mchungaji Calisto Odede wa NPC Karen, Mchungaji Francis Omondi kutoka Kenya, Dkt. Timothy Wachira, mhadhiri mkuu wa Chuo Kikuu cha Daystar, Dkt, Stanley Mukolwe kutoka Kenya, Profesa Mark Shaw kutoka Kenya, Mchungaji Elisha Onditi Odero kutoka Kenya na Eric Simiyu wa kipindi cha Hope FM cha “Yesu Ndiye Njia”.
   Kila siku ilianza kwa nyimbo za sifa na za kuabudu, kisha ukariri wa sura mbalimbali lakini mtawalia za Danieli. Ukariri ulifutwa na uchambuzi wa kitabu cha Danieli naye Mchungaji Femi Adeleye. Baada ya kusoma Biblia katika vikundi, wajumbe walitawanyika na kuingia katika vyumba tofauti ili wahudhurie warsha tofauti zilizogusia nyanja mbalimbali za maisha ya binadamu na huduma ya Injili, kwa mfano; kutafuta kazi, ufanisi masomoni, dhima ya nyimbo katika huduma, mapenzi na uhusiano,haki za kikatiba, vyombo vya habari katika huduma, urembo na mapambo, utandawazi, siasa za wanafunzi,kwa kutaja machache tu.
   Chamcha ilifuatwa na wakati wa utangamano baina ya watu na wenzao au kati yao na taasisi tofauti zilizokuwa zina maonyesho. Baada ya utangamano, wajumbe walihudhuria warsha zingine. Saa kumi unusu walirudi katika hema na kuendelea na kongamano hadi saa kumi na mbili, walipotawanyika kwa chajio. Awamu ya nne ya kongamano ilianza saa moja unusu kwa ibada na michezo ya kuigiza na kuisha saa tatu unusu.
   Mkesha wa mwaka mpya kulikuwa na tamasha la kusisimua si haba. Wajumbe kutoka karibu na mbali waliwasilisha vipawa tofauti vilivyolenga tamaduni zao. Kulikuwa na nyimbo, mavazi ya kitamaduni na mashairi.
 Wajumbe wote walishirikiana kuhesabu sekunde chache kabla ya mwaka kuruka. Uliporuka, shangwe,nderemo,mbinja na nyimbo zilitanda kote. Ungedhani ni ujenzi wa babeli. Baada ya moto wa kuruka mwaka kufifia, maombi ya mwaka yalifanywa. Hata hivyo sherehe ziliendelea baada ya maombi. Watu wana nguvu, walijitingisha na kushangalia nje ya hema hadi usiku wa manane.
CHAKULA
   Vyakula vya kiroho na vya kimwili vilikuweko kwa wingi, hata hivyo,ili mjumbe ale, lazima angemiliki kadi ya mlo, maarufu kama meal card. Sadfa ni kuwa, tulisoma Danieli 1:15 na kuona kuwa Danieli walipewa mboga na afya yao ikanawiri. Amini usiamini, hamna mlo uliokosa kabeji na sukuma wiki! Hata hivyo, Kurunzi iligundua kuwa nyama za aina tofauti zililiwa kila siku. Kinaya ni kuwa kina dada walitufeli kwani walikuwa wanashindwa kumaliza chanjo nne za mkate wa kiamsha kinywa. Nne peke yake! Chakula kilikuwa kingi hadi watu wengine wakaripotiwa kuongeza uzani.
   Chakula cha kiroho kilikuwa ni nyimbo zilizonyunyizia nyoyo za wajumbe uwepo wa Mungu, na mafunzo ya Bibilia. Kwaya iliyoundwa na wajumbe kutoka nchi tofauti ilikuwa inasifu nusura hema lipasuke. Vitabu vilikuwa vingi kwa bei nafuu, wajumbe walikuwa na ugumu wa kuchagua watakavyovinunua na pia walipewa vingine bila malipo.
   Siku ya mwisho ndiyo iliyokuwa ya kuwapeleka au kuwatuma wajumbe ili waende kubashiri. Hapo uwepo wa Mungu ukadhihirika kama mchana wa jua. Wengine waligaagaa na kutoa sauti za kunyenyekea kwa kupigwa na nguvu za Mungu. Wengine walilia kwa hisia nzito za mapenzi ya kwenda walikotumwa na Bwana na wengine walikaa kupigwa na butwaa. Uhalisia ni kwamba, Injili ina mustakabali mwema uliojaa matumaini. Bwana apewe sifa!
   Wajumbe walikuwa na matarajio mengi na ndoto nyingi zilitimizwa kwa uwezo wa Mungu. Hata hivyo waandalizi walionya hawatachukua jukumu lolote lile abadan katan katika maisha ya wajumbe baada ya kongamano.
   Hatimaye waumini wa chuo kikuu cha Moi walikuwa wengi mno hivi kwamba ungedhani uko katika bewa kuu la Chuo hiki. Kwa waliohudhuria, asanteni kwa kusikia wito, kwa waliokosa Ezra 2012 i njiani, hakikisha umehudhuria. Mungu awabariki.
   Kwa niaba ya wale wote walizipika habari hizi hadi zikaimarika, nakushukuru kwa kunipa makini na masikio yako... Hadi wakati mwingine, kwaheri. Mimi ni Paul King'ori.