Saturday 24 March 2012

KURUNZI YA KANISA FM...3


KURUNZI YA KANISA FM
  Misheni ni taashira ya zama za kale. Hata leo huendelea na matokeo yake ni ya kuridhisha na kuhuzunisha pia. Kufurahisha kwani watu hupewa matumaini ya maisha ya paradiso. Kuhuzunisha kwa sababu wengine hurudia hali zao za awali za kutenda dhambi na hivyo kufanya misheni kuzunguka tu… Mengi ninayo kutoka gatuzi la Yerusalemu na kwengine lakini kwanza tuvipate vimulimuli.
VIMULIMULI
-Yerusalemu waandamana wakiitisha rais…
-Ibada Moi sasa ni mbili…
-Huenda Yerusalemu isihitaji shilingi kufanya biashara.
Na nitakweleza yaliyojiri katika ligi ya Ukuta… Hujambo na karibu nikutaarifu, mimi ni Paul King’ori.
KURUNZI TIMILIFU
   Nchi kadhaa za Afrika zimekuwa zikipanga mapinduzi dhidi ya viongozi wao. Kwingineko Israeli wameanza kufanya maandamano huku wakiitisha kiongozi wanayemuona ili wafanane na majirani wao. Hiki ni kinyume cha sheria na kanuni walizopewa na Mungu. Alikuwa amewahakikishia kuwa yeye ndiye kiongozi au Mfalme wao, ingawa hawamuoni.
Hata hivyo, walijitetea na kusema kuwa wanafanya hivyo kwani wana wa Samweli wamekiuka maadili ya uongozi wa hekalu. Wamemkuta Samweli na kumwambia awatafutie mfalme. Walakini Samweli amesita na kuwaonya kuwa mfalme atawanyanyasa, lakini hawangesikia la mwidhini wala la mteka maji Mto Tana. Hivyo basi Samweli hakuwa na budi ila kuwapa Saulo, na kumtakasa akawa mfalme wa Israeli. Ama kwa kweli, mtoto akililia wembe, hata jembe msukumie. Ripoti ya Samweli wa Kwanza 8 na 9.
  Na huko Zarefathi, Israeli, Eliya aliendelea kufanya miujiza huku akimsaidia mjane mmoja kupata chakula wakati wa kiangazi, ila tu kwa ukarimu wa mjane huyo. Eliya aliyekuwa amewakwa na makali ya njaa, alimsihi mjane amtayarisie chakula lakini mjane akamwelezea kuwa hana chochote isipokuwa unga na mafuta kiasi mno.
  Mjane alimweleza kwamba alikuwa katika harakati za kutayarisha  chakula cha mwisho wale pamoja na mtoto wake kisha wafe njaa. Nabii Eliya alimwaahidi na kumtimizia kwani unga na mafuta hayakupungua mpaka ukame ukaisha. Hapa tunasihiwa kuwa tusivibane tulivyo navyo hata viwe vichache namna gani. Ripoti ya Wafalme wa kwanza 17:8-18.
  Yerusalemu. Yesu aliwakusanya wanafunzi wake halafu akawapa nguvu za kuzoa mashetani na kuponya ndwele. Hata hivyo, kwa vile kuugua si kufa lakini, ugonjwa ni suna, kufa ni faradhi, walitumwa kuwaauni watu katika maisha ya baada ya kifo. Wajumbe hao kumi na wawili, walipewa masharti, kutoingia kwa waliohitimu kama Wanasamaria. Ila wende kwa waliopotoka, watu wa Israeli. Jukumu lao lilikuwa ni kuhubiri ya kwamba ufalme wa mbinguni u karibu kama kesho. Waponye wanaougua, wafufue, waponye walio na shida ya ngozi na wazoe mashetani kote duniani. Baada ya hayo yote, waliagizwa kutolipisha muujiza wowote kwani walipokea bure, na bure wapeane. Mathayo 10.
Haya ni baadhi ya mambo yatakayofunzwa katika warsha ya 2011 maarufu kama Commission 2011. Warsha yenyewe itafanyika katika Chuo Kikuu Cha Kabarak kwanzia tarehe 28 Disemba 2011 hadi tarehe 3 Januari 2012. Kwa mujibu wa Nelius Wangari, ambaye anashughulikia usajili, alisema kuwa fedha zinazohitajika ni shilingi 4,900 tu!
 Hata hivyo elfu moja kati ya hizo nne ni ya sajili. Aidha, Wangari akiongea na Kanisa FM, alisema kuwa, unaweza kupata fomu ya kuchangisha pesa hizo, hivyo basi usiwe na shaka. Aliongezea kuwa pesa hizo hazilingani kamwe na thamani ya mafunzo utakayopata. Haya ni mambo utakayotumia hata maishani ya halafu. Usajili unakamilika mwisho wa mwezi huu. Pia utafunzwa jinsi ya kubashiri, yaani misheni. Je, utawachwa?
  Matukio ya hivi karibuni hapa kanisani ni kuongezeka kwa waumini. Haya yametokana na wainjilisti wa kanisa hili kujitolea mhanga na kueneza injili, karibu, mbali na kwa vyovyote vile. Waumini walitoka kila jumba na chumba na kufurika furi furi kwa ibada hadi nafasi za viti zikaadimika mno. Wengine walilazimika kuketi nje na wengine wakaamua kurudi vyumbani. Hizi ni baadhi ya sababu zilizomfanya aliyekuwa mwenyekiti, Bw. Timothy Kemboi na jopo lake kuketi kitako na kujadiliana la kufanya. Waumini walipewa fursa ya kutoa maoni yao pia.
   Asilimia kubwa ikaunga mkono dhana ya ibada mbili kila jumapili. Sasa hivi ninapopeperusha, waumini wanazo shukurani kemkem kwa uongozi wa kanisa kwa kujitolea na kuajibika katika huduma.
CHEUO…
KURUNZI BIASHARA
  Huku shilingi ya Kenya ikiendelea kupoteza thamani kwa kasi, nchi ya Yerusalemu hivi karibuni huenda ikaanza kulia kivulini. Walakini lazima wananchi wafuate masharti ya Mwenyezi Mungu. Inawalazimu kutupilia mbali dhambi zao. Kulingana na kituo cha habari cha Isaia 55:1, Wanayerusalemu wataanza kula mikate, kunywa divai na maziwa bila kulipa hata thumni? Haya yatawezeshwa na Mungu mwenyewe ili wajue kuwa yeye ndiye Mungu Muumba na kwamba yuamiliki kila kitu duniani. Wito wa usaidizi huo umepeanwa na Mola kupitia kwa msemaji wake nabii Isaia, huku akisema kuwa nia zenu si kama zake wala mawazo yake kama yenu.
KURUNZI MICHEZONI
  Katika michezo, timu ya Nehemia iliihemesha timu ya Tobia na Sanbalati huko Yerusalemu. Timu ya Sanbalati ilikuwa imekula njama ya kumchezea Nehemia vibaya na kumuua. Ilifumbuliwa kuwa Sanbalati walikuwa wamepanga kumtega Nehemia uwanjani wa kujengea ukuta. Hata hivyo Nehemia aliikwepa mikiki ya Tobia na kukataa kula mtama aliomwagiwa na akaendelea na kazi ya ujenzi wa ukuta. Hapo ndipo alipowafungia mabao nane kwa nunge kwani hawakumpata wamdhuru. Ripoti ya Nehemia 6.
 Na hapo ndipo tutakapozimia Kurunzi siku ya leo, kama kawaida ni furaha iliyoje kushikana mikono na kumulika pamoja. Hadi wakati mwingine nimekuwa wako Paul King’ori.

No comments:

Post a Comment